Injili ya Furaha ni changamoto na mwaliko wa kufanya toba, wongofu ili kuleta mabadiliko
katika maisha na utume wa Kanisa
Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, Waraka
wa Kitume Evangelii Gaudium, Injili ya Fuaraha uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko
ni changamoto na mwaliko katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa utangazaji
wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Ni waraka ambao umepokelewa
kwa mikono miwili na wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na kwamba, wanatarajia
kuufanyia kazi wakati wa mkutano wao wa kawaida, hapo Januari 2014. Baba Mtakatifu
Francisko si kwamba, amechapisha ujumbe wa Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya
kama njia ya kurithisha Imani ya Kikristo, bali ni mwaliko kwa Mama Kanisa kufanya
toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kukumbatia mabadiliko ya dhati, kama sehemu ya
mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwa kutambua kwamba, Kanisa kwa asili ni la Kimissionari.
Dr.
Tveit anasema, Waraka huu unachangamotisha na ni mwaliko kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni
ambalo hivi karibuni limehitimisha Mkutano wake mkuu uliokuwa ukifanyika mjini Busan,
Korea ya Kusini, kuanza kuufanyia kazi. Ni Waraka unaoweka uwiano bayana kati ya tafakari
kuhusu Kanisa, mitazamo ya Kimissionari na masuala ya uchumi, mazingira, haki na amani
kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa Kanisa katika mtazamo wa Kimissionari.
Baraza
la Makanisa Ulimwenguni katika mkutano wake wa kumi, lilibainisha umuhimu wa Kanisa
kufanya toba na wongofu wa ndani; kwa kuwaendea wale wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii kutokana na hali yao ya maisha na Kanisa kuanza kwa kasi na ari kubwa zaidi
mchakato wa majadiliano ya kiekumene sanjari na kusimama kidete kulinda na kutetea
misingi ya haki na amani. Hii ndiyo hija inayofanywa na Makanisa 345 wanachama wa
Baraza la Makanisa Ulimwenguni mara baada ya Maadhimisho ya Mkutano mkuu.
Kanisa
Katoliki si mwanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema Dr. Tveit, lakini
limeendelea kushirikiana kikamilifu na wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa
njia ya Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja miongoni mwa Wakristo.