2013-12-03 08:22:17

Ukweli wa kimaadili unalenga kusimamia mafao ya wengi na ustawi wa binadamu!


Mshikamano wa dhati kati ya Maaskofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kielelezo hai cha matumaini na uwepo endelevu wa Kristo miongoni mwa wafuasi wake. Mama Kanisa kwa njia ya uvumilivu wa kimama anapenda kuzima kiu ya utupu wa maisha ya kiroho na hali ya kukata tamaa miongoni mwa watu; anataka kuwasaidia waamini kutambua maana ya maisha pamoja na kuwashirikisha furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

Mama Kanisa katika maisha na utume wake, anapania pamoja na mambo mengine kuwatangazia watu wa kizazi hiki imani katika uhalisia wake; imani inayogusa undani wa maisha ya mtu na inayomwilishwa katika mikakati ya shughuli za kichungaji. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, imekuwa ni fursa ya kutangaza hazina ya imani ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Mafundisho tanzu pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa ni amana ya uzoefu na mang'amuzi ya kibinadamu, msingi wa tamaduni nyingi Barani Ulaya, unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na binadamu. Bila kuzingatia mambo haya msingi, tamaduni nyingi zitafilisika na kubaki utupu!

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko aliyotoa siku ya Jumatatu tarehe 2 Desemba 2013 wakati alipokuwa anazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Uholanzi linaloendelea na hija yake ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kuwa na uwiano wa dhati kati ya: imani na akili; ukweli na uhuru. Ukweli wa kimaadili unalenga kusimamia mafao ya wengi na ustawi wa binadamu. Kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi, Wakristo wanayo dhamana ya kuunda dhamiri nyofu, kwa njia ya majiundo makini ili kutoa uamuzi thabiti.

Ili Mama Kanisa aweze kutekeleza dhamana hii anasema Baba Mtakatifu kuna haja kwa Familia ya Mungu nchini Uholanzi kujikita katika majiundo makini na yenye ubora; kushikamana kwa dhati kutangaza kweli za Kiinjili kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na kwamba, Waamini walei wanahamasishwa kuwa ni Mitume na Wamissionari katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, ili kuweza kuyatakatifuza malimwengu.

Baba Mtakatifu anawahimiza Waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha ya hadhara kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, tayari kuwaonjesha wote huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kuleta mvuto, mashiko na matumaini kwa wale waliokata tamaa! Waamini wajikite katika majadiliano, ili kuchangia mawazo yao katika mada tete kama vile: ndoa na familia ili kutangaza Injili ya Uhai.

Majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo, yapanie kutafuta ukweli, utashi wa Mungu na majibu yanayofumbata kweli za Kiinjili, tayari kujitosa kimasomaso kukutana na wengine katika hija ya maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema, licha ya utajiri mkubwa unaopatikana nchini Uholanzi, bado kuna wimbi kubwa la umaskini linalowaelemewa watu wengi, ambao kimsingi wanahitaji kuonjeshwa mshikamano wa upendo. Maaskofu wawe makini kuhamaisha na kukea miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwani ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa Mapadre na Watawa wanaopaswa kusaidiwa ili wakue na kukomaa katika maisha ya kiroho, kiutu na kiakili. Mapadre na Watawa wakuze moyo wa: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuwa karibu zaidi na Mapadre wao katika mahitaji ya msingi, bila kuwasahau hata wale wanaolegalega katika maisha na utume wao wa Kipadre; kwani wote wanapaswa kusikilizwa kwa umakini na kuhudumiwa kikamilifu.

Baba Mtakatifu anaonesha mshikamano wake na waathirika wa nyanyaso za kijinsia, anawasindikiza katika kipindi hiki kigumu cha maisha yao, wanapojitahidi kuponya madonda ya ndani, ili waendelee kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.