2013-12-03 11:03:56

Tanzania yapata msaada wa magari 22 kutoka WHO na UNFP


Ifuatayo ni hotuba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dr. Hussein Ali Mwinyi (MB), katika hafla ya kupokea magari ya kubebea wagonjwa, yaliyotolewa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa (WHO na UNFP), tarehe 03-12-2013, katika viwanja vya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dar es salaam

Waheshimiwa Wabunge
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii

Wakurugenzi na Watendaji Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani- Tanzania
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa mataifa la Idadi ya watu- Tanzania
Wakurugenzi watendaji wa wilaya
Waganga wakuu wa wilaya
Waandishi wa habari
Wageni waalikwa

Mabibi na Mabwana,
Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kushukuru sana mashirika ya Umoja wa Mataifa yaani Shirika la Afya Duniani na Shirika la Idadi ya watu kwa jitihada kubwa zilizofanikisha kupatikana kwa magari ya kubebea wagonjwa ambayo nitayapokea hivi punde. Hivi leo nitapokea magari 20 kutoka Shirika la Afya Duniani, yaani 18 kwa ajili ya kubebea wagonjwa na magari 2 kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za Afya ya Uzazi na Mtoto katika ofisi ya Makao makuu. Pia, nitapokea magari kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu yaani magari 4 kwa ajili ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya mikoa ya Geita na Simiyu na gari 1 kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za Afya ya Uzazi na Mtoto katika mkoa wa Simiyu.

Mabibi na Mabwana,
Nina furaha kutamka kwamba Tanzania ni kati ya nchi ambazo zimefikia Lengo la Milenia namba 4, la kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa theluthi mbili ifikapo mwaka 2015. Lengo lilikuwa ni kufikia vifo 54 kwa kila vizazi hai 1,000 ingawa takwimu za mwaka 2010 zilionyesha kuwa vifo hivi vilipungua na kufikia vifo 81 kati ya vizazi hai 1,000; ripoti ya mwaka huu ya Umoja wa Mataifa imeonesha tumefikia vifo 54 kwa vizazi hai 1,000. Haya ni mafanikio ambayo yanapaswa kujivunia, pamoja na kuongeza jitihada ili kuhakikisha kwamba tunafikia lengo ifikapo mwaka 2015.

Mabibi na Mabwana,
Hata hivyo, nchi yetu bado ina changamoto ya kupunguza vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi, pamoja na vifo vya watoto wachanga. Hii inatokana na kasi ndogo ya kushuka kwa vifo vinavyotokana na uzazi. Takwimu za mwaka 2010 zinonyesha kwamba vifo vitokanavyo na uzazi ni 454 kwa kila vizazi hai 100,000, ikiwa vimepungua kutoka vifo 578 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2004/2005. Lengo ni kufika vifo 193 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2015. Kutokana na ukweli huu, nchi yetu haiko kwenye nafasi nzuri kulifikia lengo tulilojiwekea.

Mabibi na Mabwana,
Sababu ambazo zinachangia hali hii ya kasi ndogo ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni pamoja na matumizi madogo ya njia za kisasa za uzazi wa mpango (27%), upungufu wa wataalamu wanaotoa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma ya afya, na mfumo wa rufaa ya wagonjwa usiokidhi mahitaji. Upatikanaji wa magari haya 22 ya kubebea wagonjwa, umekuja wakati muafaka ambapo serikali inajitahidi kuhakikisha kwamba huduma ya afya inapatikana kwa kila mgonjwa, magari haya yataboresha mfumo wa rufaa ya wagonjwa kutoka vituo vya afya kwenda hospitali za wilaya. Ni imani yangu kwamba wale wote watakaopata magari haya watayatunza na kuyatumia kama ilivyokusudiwa.

Mabibi na Mabwana,
Katika kupambana na changamoto hizi, serikali inatekeleza mipango mbalimbali ikiwamo upatikanaji wa uhakika wa dawa za uzazi wa mpango. Aidha, udahili katika vyuo vya afya umeongezeka maradufu, katika kuhakikisha kwamba watoa huduma waliosomea wanapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma, hii ni pamoja na kuongeza uwezo wa Serikali kuajiri zaidi. Serikali inakamilisha mwongozo wa kufuatilia na kuchunguza vifo vyote vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga, ili kujua sababu ya kila kifo na kuchukua hatua stahiki, kuhakikisha kwamba vifo vinavyoweza kuzuilika havitokei tena. Aidha itakuwa ni lazima kutolea taarifa kila kifo kinachotokana na uzazi.

Mabibi na Mabwana,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Washirika wa Maendeleo, zimekarabati vituo kadhaa, ikiwa ni pamoja na zahanati, vituo vya afya na hospitali. Nia ni kuwezesha asilimia 50 ya vituo vya afya kuweza kutoa huduma za dharura za uzazi na mtoto mchanga, ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kutoa mtoto. Katika kuhakikisha hilo, Kwa siku za karibuni Wizara imesambaza vifaa vya kutolea huduma hizi katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zipatazo 780 kote nchini.


Mabibi na Mabwana,
Sera ya Afya ya mwaka 2007, Mpango Mkakati wa Tatu wa Sekta ya Afya (HSSP-III) wa 2009-15, Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) wa 2007 hadi 2017 unaolenga kuwepo kwa zahanati kila kijiji na Mpango Mkakati wa Kuongeza Kasi ya kupunguza vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano (2008-15), yote inahimiza umuhimu wa kuwa na huduma za akinamama wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua hadi siku 40 baada ya kujifungua, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano, zinazotolewa bila malipo, kwa ubora na uwiano.

Mabibi na Mabwana,
Magari haya tunayopokea leo yamegharimu jumla ya Tsh 1,617,055,527.64 sawa na Dola za kimarekani 1,006,883.89. Kati ya fedha hizo, Tsh 1,359,295,033/= (USD 846,385.45) zimegharimiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Tsh 257,760,494.64/= (USD 160,498.44) zimegharimiwa na Shirika Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA). Magari haya 22 yatagawiwa katika wilaya zifuatazo:

Hospitali ya Rufaa Mbeya (Mbeya), Hospitali ya Mkoa Manyara (Babati), Hospitali ya wilaya ya Ilemela (Ilemela), Hospitali ya wilaya ya Ludewa (Ludewa), Hospitali ya wilaya ya Chato (Chato), Hospitali ya wilaya ya Bukombe (Bukombe), Mkwajuni DDH (Chunya), Kilema DDH (Moshi).

Vituo vya afya vitakavyopokea magari haya ni: Kituo cha Afya Kirangale (Same), Kituo cha Afya Ikwiriri (Rufiji), Kituo cha Afya Pawaga (Ismani), Kituo cha Afya Bunazi (Misenyi), Kituo cha Afya Bukundi (Meatu), Kituo cha Afya Mnenia (Kondoa), Kituo cha Afya Kimeya (Muleba), Kituo cha Afya Ngarenanyuki (Meru), Kituo cha Afya Iboya, pamoja na Kituo cha Afya Masumbwe (Mbogwe), Kituo cha Afya Ikimbilo (Bariadi), Kituo cha Afya Bunambiyu (Kishapu) na Kituo cha Afya Kifanya katika mkoa wa Njombe.

Kufuatia mgao huu, naelekeza kuwa magari haya yapelekwe kwenye vituo nilivyovitaja na si vinginevyo.

Mabibi na Mabwana,
Wito wangu kwa wale wote watakaopokea magari haya ni kuwataka waweke utaratibu wa kuyafanyia matengenezo kinga ili yaweze kudumu pamoja na fedha za bajeti kwa ajili ya mafuta ili magari haya yaweze kutumika kama sera inavyoelekeza ya kuwapatia huduma bure wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Mabibi na Mabwana,
Tunapenda kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo, ambao wamekuwa nasi bega kwa bega katika nia yetu ya kuongeza ustawi wa nchi yetu, kwa upande wa afya ya mama, watoto chini ya miaka mitano na jamii kwa ujumla. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika kuboresha afya ya mama na mtoto, katika juhudi za kuhakikisha kwamba hakuna mama anakufa wakati analeta uhai, na hakuna mtoto anafariki kwa matatizo yanayozuilika.
Baada ya kusema hayo, sasa niko tayari kupokea magari ya kubebea wagonjwa

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza!!








All the contents on this site are copyrighted ©.