2013-12-03 10:05:22

Maaskofu wasikitishwa na ufisadi ulioitikisa Serikali ya Malawi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari linasema kwamba, limesali na kufanya tafakari ya kina kuhusu kashfa ya ufisadi wa fedha za umma unaofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa na uzalendo, kwa kutaka kupata utajiri wa haraka haraka, kwa njia za mkato, pasi na kuzingatia ukweli, uaminifu, uadilifu na utendaji wa kazi kwa juhudi, bidii na maarifa.

Maaskofu wanasema, ufisadi huu umepelekea wizi wa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya huduma na maendeleo kwa wananchi wa Malawi. Hili ni kundi la watu wasiokuwa na uzalendo ambalo limeitumbukiza Malawi katika shida na mahangaiko makubwa na kwamba, sera na mambo ya fedha iko mashakani kutokana na ukosefu wa maadili na ukomavu wa kiutu.

Maaskofu Katoliki nchini Malawi wanasema, ingawa kashfa hii inashughulikiwa na wadau mbali mbali, lakini wao pia wanaona kwamba, wanadhamana ya kuweza kuchangia mawazo yao kwa kuzingatia madhara yanayosababishwa na ufisadi huu unaoendelea kuyatumbukiza mamillioni ya watu katika umaskini wa hali na kipato, kwa kukosa sera makini zinazotoa kipaumbele kwa binadamu na maendeleo yake.

Msimamo wa wafadhili kutochangia tena bajeti ya Serikali ya Malawi, utasababisha madhara makubwa ya kiuchumi kwa ongezeko kubwa la bei za bidhaa na huduma. Malawi itakosa fedha za kigeni kugharimia huduma mbali mbali hali ambayo itasababisha majanga kwa wananchi wa kawaida! Ni wananchi ambao wameporwa fedha zao na kwamba, wataendelea tena kuteseka kwa kukosa huduma msingi za maendeleo na huduma za kijamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linasema, kuna haja kwa Serikali kufanya uchunguzi wa kina na wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu shutuma zinazowakabili, ili kujenga tena uaminifu kwa wananchi wa Malawi pamoja na wafadhili kutoka nje. Serikali ya Malawi ikiri uwajibikaji wake wa kimaadili na fedha iliyoibwa irudishwe kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Malawi. Serikali iwe makini kusikiliza kilio cha wananchi wa Malawi wakati huu wa mtikisiko wa uchumi nchini Malawi.

Maaskofu wanawaomba wafadhili kuendelea kuchangia katika bajeti ya Serikali ya Malawi kwa ajili ya maendeleo ya watu wa kawaida. Wananchi watubu na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu; wajitahidi kuongozwa na Amri za Mungu na dhamiri nyofu, tayari kujitoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Malawi. Serikali iwe makini katika kudhibiti fedha ya umma na kuwawajibisha mafisadi bila huruma. Kanisa liwe mstari wa mbele kuhamasisha moyo wa uzalendo na uwajibikaji.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linalaani kwa nguvu zote ufisadi, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma unaofanywa na watu wachache waliopewa dhamana ya kusimamia maendeleo ya watu. Hiki ni kitendo ambacho ni kinyume kabisa cha maadili, changamoto kwa wananchi wa Malawi, kutubu na kumwongokea Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.