2013-12-03 09:39:38

Kuna matumaini katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi, lakini bado kuna mengi ya kufanywa!


Ugonjwa wa Ukimwi bado unaendelea kuwa ni tishio kwa familia nyingi Barani Afrika, licha ya maendeleo makubwa yaliyokwisha kupatikana katika utoaji wa dawa za kurefusha maisha. Waathirika wakubwa ni wanawake wanaolazimika kubeba mzigo wa huduma kwa familia zao wakati wa shida na mahangaiko ya kuwatunza wagonjwa wa Ukimwi.

Bwana Ban Ki- Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Matifa katika ujumbe wake wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2013 anasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ina matumaini makubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na kwamba, kuna watu millioni 14 ambao watapatiwa dara za kurefusha maisha hadi kufikia Mwaka 2015. Anasema, bado kuna tatizo la unyanyapaa miongoni mwa watu na kwamba, kuna haja ya kuhakikisha kuwa watu wengi zaidi wanapata dawa za kurefusha maisha.

Udhibiti wa maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto ni jambo la muhimu sana, wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapojizatiti kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi. Mkakati huu hauna budi kwenda sambamba na heshima kwa wanawake, kwa kukomesha vitendo vyote vinavyowasababishia madhulumu na nyanyaso pamoja na kuwakinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, hayana budi kwenda sanjari na vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria na Kifua Kikuu; magonjwa yanayoendelea kusababisha vifo vya watu wengi duniani, lakini zaidi miongoni mwa wananchi wanaotoka katika nchi maskini zaidi duniani. Jumuiya ya Kimataifa inayo kazi kubwa mbele yake ili kuhakikisha kwamba, Ukimwi unatokomezwa kutoka katika uso wa dunia!







All the contents on this site are copyrighted ©.