2013-12-03 11:37:02

Kanisa linatumwa kutangaza Injili ya Furaha inayomkirimia mwanadamu: amani, utulivu n afuraha ya ndani!


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Francisko Xsaveri, Mtume wa Uinjilishaji nchini India na msimamizi wa shughuli za kitume duniani. Mama Kanisa anatumwa ulimwenguni kutangaza Injili ya Furaha inayomkirimia mwanadamu amani, utulivu na furaha ya ndani. Watu wana kiu ya amani itakayoletwa na Masiha.

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican siku ya Jumanne. Anasema, Injili inamwonesha Yesu akiwa amesheheni furaha wakati alipokuwa anahubiri, alipokuwa anawaponya wagonjwa na kusali kwa Baba yake wa mbinguni. Amani inayobubujika kutoka katika undani wa Kristo inapaswa kuwafikia watu wengi zaidi kwani ni furaha inayojika katika utulivu wa ndani.

Furaha ya Mama Kanisa ni kutangaza Habari Njema kwamba, Yesu ni Bwana na Mwokozi wa Mataifa, waamini wanapaswa kuonja na kuendelea kukua na kukomaa katika furaha hii wanayowashirikisha jirani zao. Amani inayoletwa na Yesu Kristo Masiha ni amani ya furaha na sifa kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu ambalo limefunuliwa kwa watoto wadogo na wanyenyekevu wa moyo! Kanisa ni kielelezo cha matumaini kwa wale waliokata tamaa na kwamba, linatumwa kutangaza Injili ya Furaha hadi miisho ya dunia!







All the contents on this site are copyrighted ©.