2013-12-02 14:33:02

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 2 Desemba 2013 amekutana na kuzungumza na Bwana Benjamin Netanyahu, Waziri mkuu wa Israeli, ambaye baadaye alikutana na kuzungumza pia na Askofu mkuu Pietro Parolin aliyekuwa ameandamana na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Mazungumzo ya viongozi hawa wawili yamejikita katika hali tete ya kisiasa na kijamii Mashariki ya Kati, lakini kwa namna ya pekee harakati za Jumuiya ya Kimataifa kurudisha tena majadiliano kati ya Israeli na Palestina, kwa kuonesha matumaini kwamba, suluhu ya kudumu kati ya pande zote mbili ni kulinda na kuheshimu haki za nchi husika.

Baba Mtakatifu na Waziri mkuu wamegusia pia hija ya kichungaji kwa Baba Mtakatifu Francisko nchini Israeli pamoja na masuala kadha wa kadha, yakiwemo: uhusiano kati ya Serikali na Jumuiya za Kikristo; uhusiano kati ya Israeli na Vatican na kwamba, itifaki ya makubaliano inayoendelea kufanyiwa kazi na pande hizi mbili itaweza kukamilika haraka iwezekanavyo.







All the contents on this site are copyrighted ©.