Waraka wa Kitume: Injili ya Furaha: Evangelii Gaudium: kwa muhtasari
Waraka wa Kitume Injili ya Furaha, “Evangelii Gaudium” uliochapishwa na Baba Mtakatifu
Francisko unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini
kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu
kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa
kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya.
Askofu mkuu Rino
Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anasema,
Waraka huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji unaopaswa
kutekelezwa na Mama Kanisa kwa siku za usoni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo
chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume
wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi.
Waraka
huu wa kitume unachota utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi
juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo. Baba Mtakatifu
Francisko, akayasoma na kuyafanyia tafakari ya kina na hatimaye kuyaweka kuwa ni sehemu
ya ujumbe wake kwa Familia ya Mungu wakati huu inapojielekeza katika hija ya Uinjilishaji
Mpya, kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ndiye kiini cha Uinjilishaji na ndiye Mwinjilishaji
Mkuu. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa
na Yesu mwenyewe katika mazingira mapya ya Uinjilishaji.
Baba Mtakatifu katika
mwono huu wa Kimissionari ambao ndio msingi wa Waraka huu wa kitume anaugawa sehemu
kuuu mbili. Sehemu ya kwanza ni mwaliko kwa Makanisa mahalia kuangalia changamoto
na fursa zilizopo mintarafu tamaduni na hali halisi ya nchi husika. Baba Mtakatifu
anatoa kigezo kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu na kwa kila mdau wa Uinjilishaji,
ili kwa pamoja kuwa na mbinu shirikishi katika mchakato wa Uinjilishaji pasi na kujitenga
kama kisiwa!
Baba Mtakatifu Francisko anabainisha nguzo kuu saba za Uinjilishaji
zinazopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mwono wa Uinjilishaji Mpya: Mageuzi
ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, Kanisa kimsingi ni la Kimissionari; vishawishi
vya Wainjilishaji, Kanisa kama Familia ya Mungu inayotumwa Kuinjilisha; mahubiri na
matayarisho yake; ushiriki wa kijamii wa maskini katika maisha na utume wa Kanisa;
amani na majadiliano ya kijamii na kiini cha kazi ya Uinjilishaji inayofanywa na Mama
Kanisa. Yote haya yanafumbatwa kwa umakini mkubwa katika huruma na upendo mfunuliwa
wa Mungu unaogusa moyo wa kila mtu kwa kukutana na Yesu, chemchemi ya furaha inayomsukuma
mwamini kushirikisha upendo huu kwa wengine.
Baba Mtakatifu Francisko katika
Sura ya kwanza ya Waraka wa Kitume: Injili ya Furaha anasema kwamba, mabadiliko
yanayopaswa kufanywa na Mama Kanisa ni kutokana na utambuzi kwamba, Kanisa kwa asili
ni la Kimissionari, linalofanya hija ya kutoka katika undani wake ili kukutana na
Yesu, kwa kutambua kwamba, waamini katika hija hii wanaambatana na Mungu ambaye analionesha
Kanisa dira na njia ya kufuata nyayo za Kristo, daima likiwa limesheheni huruma.
Ili
yote haya yaweze kutekelezeka, kuna umuhimu wa kuwa na wongofu wa kichungaji unaolitaka
Kanisa kuendeleza kazi ya Uinjilishaji kwa kuachana na miundo mbinu ya Kanisa inayoweza
kuwa ni kikwazo cha dhamana hii. Wadau wa Uinjilishaji Mpya waoneshe ugunduzi na kuibua
mikakati kadiri ya tafiti makini zilizofanywa katika eneo husika, ili kubainisha malengo
maalum yanayopaswa kufikiwa na Jumuiya husika kwa kuzingatia mambo msingi tu! Kujenga
hierakia za ukweli mintarafu kiini cha Injili inayofumbata upendo. Kunatakiwa kuwepo
na uwiano sawa kati ya hazina ya imani na lugha inayotumika, wakati mwingine, lugha
inaweza kushindwa kufikisha Kweli za Kiimani.
Baba Mtakatifu katika Sura ya
kwanza anawaalika kwa namna ya pekee Waamini kuhakikisha kwamba, wanamwilisha katika
maisha na utume wa Kanisa matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican;
kuangalia upya dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki hususan katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Wainjilishaji watambue
mapungufu yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya lugha ya mwanadamu na kwamba
wanapaswa kutambua utajiri unaofumbatwa katika Hazina ya Imani.
Baba Mtakatifu
Francisko katika Sura ya Pili ya Waraka wa Kitume, Injili ya Furaha, Evangelii
Gaudium, anachambua kwa kina na mapana changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa
Uinjilishaji Mpya. Jambo la msingi ni kuondokana na dhana ya kujisikia wanyonge, hali
inayoweza kusababisha Wainjilishaji kushirikisha furaha yao kwa wengine kwa njia ya
ushuhuda wa maisha.
Uinjilishaji uwe ni sehemu ya mchakato unaomwezesha mwamini
kukua na kukomaa na kwamba, magumu anayokutana nayo yasiwe ni sababu ya kumkatisha
tamaa. Wawe makini na matumizi ya teknolojia na utandawazi; kwa kuondokana na mambo
yanayosababisha mpasuko wa kijamii kwa kupenda mno fedha na mali; madaraka na heshima;
mmong’onyoko wa tunu msingi za maadili na utu wema; soko huria kupewa kipaumbele cha
kwanza. Kanisa halina budi kuendeleza matendo ya huruma na mshikamano kwani hii ni
sehemu ya maisha na utume wake miongoni mwa watu wa Mataifa.
Baba Mtakatifu
Francisko anasema kwamba, Uinjilishaji Mpya katika nyakati hizi unakabiliana na changamoto
zinazoibuliwa na tamaduni za miji, changamoto kwa waamini kutokubali kumezwa na malimwengu;
ukanimungu na mafundisho potofu; imani inayofanya rejea kwa maisha binafsi na kwamba
neema inaweza kupatikana kwa kutumia mabavu. Haya yote ni makwazo katika Uinjilishaji
mpya, mambo ambayo yanapaswa kung’olewa kabisa kwa kukazia ushuhuda wa umoja unaojionesha
kwa kukamilishana. Wanawake na waamini walei wanapaswa kushirikishwa kwa namna ya
pekee katika maisha na utume wa Kanisa, ili waweze kuchangia katika ujenzi wa Kanisa.
Sura
ya tatu ya Waraka wa Injili ya Furaha, Evangelii Gaudium, Baba Mtakatifu anaelezea
kwamba, Uinjilishaji ni dhamana ya Familia nzima ya Mungu kwa kutambua neema ya Mungu
inayofanya kazi kwa Wainjilishaji wote. Anakazia umuhimu wa kuendeleza utamadunisho
kwani Injili haina utambaulisho wa utamaduni maalum sanjari na kukazia mahusiano ya
ya kijamii kati ya watu kama njia ya ushuhuda wa Kweli za Kiinjili.
Baba Mtakatifu
anawahimiza watu kukuza na kuendeleza Ibada mbali mbali, kielelezo cha ushuhuda wa
imani kwa wale ambao wameonja na kuguswa na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mwishoni
mwa surah ii, Baba Mtakatifu anawaalika wanataalimungu kutafuta mbinu mkakati utakaosaidia
watu kufurahia njia mbali mbali za Uinjilishaji.
Mahubiri ni sehemu muhimu
sana katika Uinjilishaji Mpya, jambo linalohitaji moyo na ari ya kulipenda Neno la
Mungu na Watu wa Mungu wanaowahubiria: Mahubiri yawe mafupi na wala yasiwe ni “majigambo”
ya kisomi; yawe ni mawasiliano yanayogusa sakafu ya moyo ya mwamini na wala yasiwe
ni mahali pa kuwakaripia watu. Wainjilishaji wajiandae kikamilifu, ili mahubiri yao
yawaletee watu matumaini na kamwe yasiwatumbukize katika mwono potofu! Neno la Mungu
lifundishwe kwa kuwaojengea waamini mwono sahii kwamba linaweza kugusa undani wa maisha
yao; linajengeka katika majadiliano, uvumilivu na ukarimu bila ya kuhukumu.
Sura
ya nne ya Waraka wa Kitume, Furaha ya Injili, Evangelii Gaudium, Baba Mtakatifu
Francisko anaelekezea kwa kina na mapana kuhusu mwelekeo wa uchumi kimataifa unaojikita
katika misingi ya ukosefu wa haki, hali ambayo inapelekea wanyonge kuendelea kunyong’onyea
katika Jamii na wenye nguvu kufurahia maisha. Utamaduni wa kutojali na kuguswa na
mahangaiko ya jirani umeunda kundi kubwa la watu wanaonyonywa na hatimaye, kusukumizwa
pembezoni mwa Jamii zao, kama “makapi”. Soko huria ni kati ya nguvu kuu ambayo imeibuka
katika Jumuiya ya Kimataifa; watu wanatafuta faida kubwa, rushwa na ufisadi yanaonekana
kuwa ni mambo ya kawaida kiasi cha baadhi ya watu kukwepa kulipa kodi kwa makusudi
kabisa pamojana na madhulumu na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo.
Katika
sehemu hii, Baba Mtakatifu anaunganish dhamana na umuhimu wa Uinjilishaji pamoja na
huduma ya maendeleo kwa mtu mzima, tayari kutolea ushuhuda wa imani katika maisha
binafsi na kwenye hadhara. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, analichangamotisha Kanisa
kuhakikisha kwamba, linawahusisha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii
katika maisha na utume wake. Kanisa liendelee kusimama kidete kulinda na kutetea misingi
ya haki na amani kwa njia ya majadiliano ya kijamii. Maskini wanayo mengi ya kulifundisha
Kanisa na kwamba, kuna haja ya kuibua mbinu mkakati kwa ajili ya kupambana na umaskini
wa hali na kipato miongoni mwa watu.
Anawaalika wanasiasa pia kulivalia njuga
baa la umaskini kwa kuwa na sera na mikakati makini kwa ajili ya watu wao. Kanisa
ni Jumuiya ya waamini, kamwe hawapaswi kuwasahau maskini wanaoishi nao! Baba Mtakatifu
analihamasisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linawahudumia: wakimbizi na wahamiaji; watu
wasiokuwa na makazi maalum; wazee wanaotelekezwa na kukumbwa na upweke hasi, ambao
idadi yao inaongezeka maradufu. Watumwa wa biashara ya utumwa mamboleo wanapaswa kusaidiwa.
Kuna watu wanaoteseka kutokana na tabia ya baadhi ya watu kukumbatia utamaduni
wa kifo na sera za utoaji mimba; hawa ni watu ambao utu wao una nyanyasika. Kuhusu
sera za utoaji mimba, Kanisa halitabadili mafundisho yake kwani ni jambo linalokwenda
kinyume na zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kanisa halina budi kusimama kidete
kulinda na kutetea Injili ya Uhai, utu na heshima ya binadamu na kwamba, hii ni dhamana
ya wote.
Baba Mtakatifu anakazia umoja dhidi ya kinzani na mafarakano; ukweli
dhidi ya mawazo ya kufikirika; mambo msingi katika mchakato wa majadiliano yanayoweza
kusaidia kujenga na kudumisha misingi ya amani katika medani mbali mbali za maisha
ya mwanadamu: yaani katika masuala ya Kisayansi, Kiekumene na Kidini. Yote hii ni
misingi ya Uinjilishaji Mpya ili kujifunza maana kutoka kwa wengine: umuhimu na maana
ya mshikamano wa Maaskofu; umuhimu wa Sinodi; haki na amani kama sehemu ya mchakato
wa Uinjilishaji pamoja na kuachana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, kwani
imekuwa ni chanzo cha uvunjifu mkubwa wa amani sehemu mbali mbali za dunia.
Sura
ya tano ya Waraka wa Kitume, Injili ya Furaha, Evangelii Gaudium, Baba Mtakatifu
anazungumzia kuhusu Roho ya Uinjilishaji Mpya, dhamana inayotekelezwa chini ya usimamizi
wa Roho Mtakatifu, anayewawezesha wainjilishaji kujikita katika sala na tafakari ya
kina kwa kutambua dhamana na nafasi ya Bikira Maria nyota ya Uinjilishaji Mpya. Mama
Kanisa anachangamotishwa katika siku za usoni, kujikita katika azma ya Uinjilishaji
Mpya kwa: ari, moyo mkuu na furaha ili kushuhudia upendo endelevu wa Kristo bila kukatishwa
tamaa na vizingiti vya maisha. Ni wainjilishaji wanaotekeleza utume wao kwa njia ya
Sala na Kazi, ili kumtangaza Yesu Kristo kwa Watu wa Mataifa.
Lugha anayotumia
Baba Mtakatifu Francisko inawagusa watu kutoka katika undani wa maisha yao. Mama Kanisa
anahimizwa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinaonesha hali halisi katika
azma ya Uinjilishaji Mpya, ili Injili ya Kristo iweze kuwafikia watu wengi zaidi,
ingawa kuna baadhi ambao wamebahatika kusikia kwa kina zaidi.
Kanisa linatumwa
kuwaendea maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii; wagonjwa na wale waliosahaulika.
Kanisa lijifunze kutafakari na kumwabudu Mwenyezi Mungu, tayari kumtolea ushuhuda
wa imani tendaji. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kutambua kiini cha imani yao
kuwa ni Yesu Kristo Mfufuka na Kanisa ambalo linaonesha huruma kwa watu wa nyakati
hizi wenye kiu ya kuonana na Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha
Waraka wa Kitume, Injili ya fuaraha, Evangelii Gaudium kwa Sala ya Bikira Maria, Mama
wa Uinjilishaji Mpya ambaye kwa mtindo wake wa maisha, Kanisa linapenda kuendeleza
dhamana ya Uinjilishaji. Kila mwamini anayemtaza Bikira Maria awe mshiriki wa mageuzi
ya upendo na huruma.
Muhtasari huu umeandaliwa na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.