2013-12-02 08:20:37

Msijirushe mkasahau kukesha!


Desemba Mosi, Mama Kanisa amekianza kipindi cha Majilio, yaani Jumapili ya kwanza ya Majilio. Hiki ni kipindicha subira, matarajio ya ujio wa nafsi ya pili ya Mungu - Yesu Kristo katika maisha yetu ya Kiroho.

Waamini wanakumbushwa kwamba, Ujio wa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia unaweza kuangaliwa katika matukio makuu matatu: Katika Fumbo la Umwilisho, Atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho na tatu; Yesu anakuja kila siku katika maisha ya mwamini kwa njia: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na waamini wanapomwilisha Injili ya Furaha kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Padre Beno Michael Kikudo kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam anatushirikisha tafakari ifuatayo:
Tunapoanza kipindi hiki cha Majiliotunapata mwaliko huu kutoka kwa Mungu:

1. Kufua mapanga yetu, sime na silaha za maangamizi ili ziwe vitu vya amani na maendeleo. Nimwaliko wa kufua hasira yetu ili iwe upendo. Mwenye hasira ana nguvuya kuweza kuua au hata kuharibu kilicho mbele yake. Nguvu hiyo hiyo
ibadilishwe na iwe kitu cha kupenda, kujali, kufariji, kusamehe na
kuinua wengine. Somo la kwanza, (Isaya 2:1-5) ".. watafua mikuki yao
iwe majembe ya plau.." ni kuonesha uwezekano wa kuleta furaha, maendeleo, ustawi kwa nguvu tulizonazo za kiakili na kimwili.

Tudhamirie katika kipindi hiki cha Majilio - familia zetu zisijifunze vita, ugomvi, wala matukano. Nguvu ndogo tuliyonayo tutumie kwa kulima bustani, tufue nguo, tusaidie wagonjwa na wenye shida. Nguvu hii itumike kwa michezo na kukuza vipaji kwa vijana.

2. Maisha yetu ya kiroho daima yawe macho na tayari. Mfano anaotoa Kristo
ni ule wa wakati wa Nuhu - (Mt 24:37-44). Watu walisema, "acha tujirushe", au "ponda mali kufa kwaja.." Waliendelea na maisha yao ya
anasa wasing'amue mpango na mwaliko wa Mungu. Gharika ilipokuja wote wakafa. Kwetu sisi isiwe hivyo. Bali tujiandae kwa kuzivaa silaha za kiroho kwa sala, kulitafakari neno la Mungu, na kuzitumia kila nafasi tukutanapo na mhitaji iwe kama vile tumekutana na Kristo mwenyewe. Kwa maana yeye atatuambia mwisho wa nyakati"nilikuwa na njaa mkanipachakula.."

Msisitizo wa kuwa macho pia anatukumbusha Mtume Paulo katika somo la
pili. Paulo anatukumbusha tusipatwe na siku hiyo ghafla kama mwizi.Tuwe tayari wakati wote (Warumi 13:11-14) Mungu Baba atubariki kila mmoja wetu ili tuanze Majilio hii vizuri na kuweza kujichotea Neema na Baraka tele kutoka kwa Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.