Maisha ya Kikristo ni hija ya upendo, udugu na mshikamano wa dhati kumwendea Kristo!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, majira ya jioni
alitembelea Parokia ya San Cirillo Alessandrino, iliyoko nje kidogo ya mji wa Roma.
Parokiani hapo ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Takatifu sanjari na kutoa Sakramenti
ya Kipaimara kwa vijana tisa. Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, maisha
yao ni hija ya kumwendea, ili hatimaye kukutana na Yesu Kristo, chemchemi ya furaha,
amani na matumaini mapya, kwani Kristo aliyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa
mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Waamini wanakutana na Yesu
katika maisha ya Sala, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma. Amewakumbusha Wakristo
walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kwamba, huo si mwisho wa kuuona mlango
wa Kanisa kama wanavyofanya vijana wengi, lakini hii inapaswa kuwa ni mwendelezo wa
hija ya kutaka kukutana na Yesu katika maisha ya kila siku kwa njia ya maisha adili
na matendo mema. Baba Mtakatifu anasema, kwake ni furaha ya pekee kwani anaungana
na waamini wengine kutembea ili kukutana na Yesu.
Maisha ya Kikristo ni hija
ya upendo, udugu na mshikamano wa dhati ili kumwendea Kristo, anayepaswa kuwa ni kiongozi
mkuu anayewaongoza waamini kwa upendo mkuu; anawajalia Sakramenti ya Upatanisho ili
kuonja tena huruma na upendo wa Mungu, pale wanapojikuta wakitumbukia katika dhambi.
Yesu ni tabibu wa kweli anayemponya mwanadamu kiroho na kimwili. Jambo la msingi kwa
kila mwamini kutambua kuwa ni mdhambi, anayehitaji kuonjeshwa huruma na upendo wa
Mungu kwa njia ya Kristo.