Jimbo kuu la Songea, Tanzania linaloundwa na Majimbo ya: Iringa, Lindi, Mbeya, Mbinga,
Njombe na Tunduru- Masasi linasherehekea Jubilee ya Miaka 25 tangu lilipoanzishwa
na Mwenyeheri Yohane Paulo II, kunako tarehe 18 Novemba 1987.
Kilele cha Maadhimisho
haya hapo tarehe Mosi Desemba 2013, kimekwenda sanjari na Maadhimisho ya Kufunga Mwaka
wa Imani, katika Ibada iliyoongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Msimamizi wa
Kitume wa Jimbo kuu la Songea ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Jimbo kuu la Songea lilibahatika kutembelewa na Mwenyeheri Yohane Paulo II, Septemba,
1990.
Katika mahubiri yake, Askofu Ngalalekumtwa amewataka waamini kujiandaa
vyema ili kushiriki kikamilifu katika kipindi cha Majilio, kwa kufanya toba na wongofu
wa ndani, tayari kumpokea Yesu Kristo Masiha anayekuja kuwatembelea katika maisha
yao.
Askofu Ngalalekumtwa anasema, Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia
ya tatu ya Ukristo inayojielekeza zaidi katika Uinjilishaji Mpya, waamini wanapewa
nyenzo za kufanyia kazi kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Amewataka
waamini kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu kama njia ya kufika mbinguni.
Wamepewa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa Imni, Sakramenti
za Kanisa, Maisha adili na Maisha ya Sala, ni jukumu lao kuifahamu ili kutolea ushuhuda
wa imani tendaji katika uhalisia wa maisha. Waamini wamekabidhiwa Nyaraka 16 za Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican, wanazopaswa kuzifanyia kazi.