Changamoto zinazolikabili Kanisa Visiwani Antilles
Visiwa vya Caribbean ni kati ya maeneo ya Amerika ya Kusini yaliyobahatika kusikia
Habari Njema ya Wokovu, yapata miaka 400 iliyopita. Visiwa hivi vinaundwa na watu
kutoka katika lugha na tamaduni mbali mbali; watu ambao wana mielekeo tofauti ya kiuchumi
na kijamii; historia na mwono wa maisha, mambo ambayo yasipoangaliwa kwa umakini mkubwa
yanaweza kukwamisha mchakato wa Uinjilishaji Mpya Amerika ya Kusini.
Kanisa
katika Visiwa hivi linakabiliwa na changamoto ya: upungufu mkubwa wa Mapadre na Watawa;
kupungua kwa waamini wanaojitoa kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa pamoja
na ukata unaokwamisha mikakati ya mipango ya maendeleo: kirohio na kimwili.
Hizi
ni changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi, kwani Kanisa bila Mapadre, litachechemea
katika shughuli mbali mbali za kichungaji: kiroho na kimwili. Maaskofu wanahaja ya
kuwekeza zaidi katika kuhamasisha na kulea miito ya maisha ya Kipadre na Kitawa. Lengo
hili linaweza kufanikiwa ikiwa kama vijana wa kizazi kipya wataonja furaha, ari na
uaminifu wa Mapadre katika maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake.
Ni
maneno ya Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji
wa watu, alipokuwa anazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki kutoka katika Visiwa
vya Antilles, hivi karibuni wakati wa hija yake ya kichungaji nchini humo. Anasema,
kuna uhaba wa Wakristo kutokana na ukweli kwamba, kuna makundi makubwa ya watu wanahama
ili kutafuta fursa mpya za ajira; uhaba wa wahudumu wa Injili, na huduma hafifu zinazotolewa
kwa waamini ni kati ya mambo yanayochangia baadhi ya waamini kukosa dira na mwelekeo
katika maisha na utume wa Kanisa, matokeo yake ni waamini wengi kukimbilia katika
Madhehebu ya Kikristo yanayoendelea kushamiri kwa kasi kubwa Amerika ya Kusini.
Kanisa
Katoliki anasema Kardinali Filoni linaanza kupoteza utambulisho wake katika huduma
za elimu na afya kwa kukosa wahudumu makini, jambo ambalo ni hatari kwa maisha na
ustawi wa Kanisa. Maaskofu wanaalikwa kuwekeza zaidi katika majiundo ya waamini walei
kwa njia ya vyama vya kitume, ili kuleta ari na mwamko mpya katika maisha ya Kanisa
nchini humo.
Waamini bado wanahamasishwa kuchangia katika harakati za kulitegemeza
Kanisa mahalia na kwamba, viongozi wa Kanisa waongozwe na ukweli na uwazi katika matumizi
ya rasilimali na mali ya Kanisa. Maaskofu kamwe wasikate tamaa, bali wajifunge kibwebwe
kutafuta tiba ya matatizo na changamoto hizi.
Maaskofu waguswe na mahitaji
ya Mapadre wao na wawe tayari kuwaonesha upendo na huruma ya kibaba! Wajitahidi kuwapatia
fursa za majiundo endelevu katika shughuli za kichungajik, maisha ya kiroho na kitamaduni.