Mikakati ya SECAM na CCEE kati ya Mwaka 2015 - 2017
Tume ya ushirikiano kati ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na
Madagascar, SECAM pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya, CCEE, katika
mkutano wao uliokuwa unafanyika mjini Roma, wameamua kufanya semina ya pamoja kati
ya Maaskofu kutoka Barani Afrika na Ulaya, itakayofanyika mwezi Mei, 2015.
Itakuwa
ni fursa kwa Maaskofu hawa kuweza kufanya tafakari ya kina kuhusu Waraka wa Kitume:
Injili ya Furaha, Evangelii Gaudium uliotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko
pamoja na changamoto zinazojitokeza katika maisha ya ndoa na familia, mambo yatakayojadiliwa
kwa kina na mapana wakati wa Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya
Familia, itakayofanyika mjini Vatican, mwezi Oktoba 2014.
Washiriki katika
semina hii watajikita zaidi katika changamoto ya kutangaza Furaha ya Familia. Maaskofu
wataangalia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia Barani Afrika na Ulaya. Hii inatokana
na ukweli kwamba, Familia ni wadau wakuu wa mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Familia
pia zinapaswa kuinjilishwa ili ziweze kutekeleza wajibu na dhamana yake kikamilifu
katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu hawa pia watakuwa na semina kunako mwaka
2017.
Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada
ya Kanisa Katoliki Cor Unum ameshiriki kwenye kikao cha kamati ya ushirikiano kati
ya SECAM na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya.