2013-11-30 07:42:06

Kipindi cha Majilio!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, leo kama Kanisa tunaadhimisha mwanzo wa kipindi cha majilio ili kukumbuka jinsi Mungu alivyo waongoza na kuwatayarisha wazee wetu katika imani ili kumpokea Mkombozi wetu Yesu Kristo. RealAudioMP3

Mwanzo huu wa majilio tunaweza kuutafakari na kuulinganisha na busara katika misemo yetu itufundishayo kuwa: «Mbiu ya mgambo ikilia basi ujue ina jambo!» Kanisa kokote duniani leo linapuliza mbiu kutualika kumshukuru Mungu kwa kutujalia kuanza kipindi cha majilio, kipindi cha kujiandaa kumpokea Bwana na mwana mzaliwa Yesu Kristo. Kipindi cha majilio kinakuwa pia ni mwanzo wa mwaka mpya wa kikanisa, mwaka wa imani, au mwaka wa kiliturujia.

Kwa namna ya pekee, kanisa tena lina mshukuru Mungu kwa kutujalia kumaliza mwaka wa maadhimisho kiimani huku tukiwa salama, tena wenye furaha kubwa. Ni Mungu katulinda hadi leo na katujalia kuyaishi, kuyaonja na kuyavuna yale yote yaliyo mazuri; hivo hatuna budi kumtolea shukurani kemkem na kwa dhati. Kati ya matukio mengi ya kufurahisha ni kumbukumbu ya kutangazwa na kuzinduliwa mwaka tunaoumaliza kama mwaka wa imani na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI.

Hatunabudi kumshukuru Mungu kwa yote na tena tuzidi kuomba wingi wa baraka, neema na rehema kwa Mwaka huu tunao uanza leo kikanisa. Kwa furaha hii sinabudi kuwatakieni heri ya mwaka mpya, wapendwa wakristo wote na watu wote wenye mapenzi mema popote pale mlipo.

Mpendwa msikilizaji, Mwaka wa Kanisa ki-maadhimisho umegawanyika katika vipindi vikuu viwili: yaani «Krismas na Pasaka». Krismas inaanza na kipindi chake cha maandalizi yaani «Majilio» na kuendelea katika kipindi cha mwendelezo wake hadi Epifania au sherehe ya tokeo la Bwana. Paska inaanza na kipindi chake cha maandalizi yaani «Kwaresma» na kuendelea katika kipindi cha mwendelezo wake hadi sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, wakatoka kifua mbele kutangaza Injili ya Furaha.

Kama vile Kwaresma ilivyo kipindi cha maandalizi ya Pasaka, ndivyo Majilio ilivyo kwa Krismas. Katika wakati wote huu wa kuishi na kujiandaa kwa sherehe na sikukuu za Krismas; yatupasa kuwa karibu na Yesu mwenyewe aliye asili, kiini na kilele cha maadhimisho yote ya kanisa. Kwa hivyo Majilio na vipindi vingine vyote katika mwaka wa Kanisa si kitu kingine bali ni maisha ya wakristo na namna yao ya kumwadhimisha Kristo katika mafumbo yake ya ukombozi ndani ya kusanyiko na maisha binafsi ya kila mbatizwa. Majilio kwa wabatizwa: ni kujiandaa kumpokea Kristo Maishani na rohoni; kuishi kama Kristo au kuwa Kristo mwingine (alterius Christus) kwa matendo mema, sala, toba na mfungo.

Mpendwa msikilizaji, tunaweza kusema kuwa, majilio ni ufunguo wa kuanza mwaka wa kanisa. Yaani kuanzia sasa: kanisa litamwadhimisha na kumwona Kristo kama mtoto mzaliwa pangoni Bethlehemu - Krismas (Matayo 2: 1-12), Kristo kijana akifunga jangwani na kujiandaa kwa safari yake ya ukombozi- Kwaresma (Matayo 4: 1-11), Kristo akiteswa na kufa msalabani (Matayo 27: 27-31; 27: 45-50), Kristo akifufuka kutoka wafu na kushinda kifo na dhambi (Matayo 28: 1-7), Kristo akiwatokea na kuwahudumia mitume na wafuasi wake (Yohane 21: 13), Kristo akikabidhi kanisa lake kwa mitume na wafuasi ili waendeleze kazi yake (Yohana 21: 15-18), Kristo akipaa na kuketi mbinguni kuume kwa baba (Matendo 1: 6-11), na mwisho Kristo akimtuma na kumshusha Roho Mtakatifu kwa mitume na wafuasi wake (Matendo 2: 1-41). Namna hii yote ina nia moja tu, yaani kuadhimisha historia ya wokovu na ukombozi wetu.

Majilio hutufungulia hazina ya upendo wa Mungu kwa kutugeuza zaidi na zaidi tuzidi kufanana na Kristo Yesu. Kwa namna hiyo katika mwaka wa kanisha tutamwona Bwana Yesu Kristo akipita tena kati yetu akitukomboa kwa kutenda mema na akitujalia hadhi na heshima ya kuwa wana wa Mungu (Yohane 1: 12). Hii ndiyo Noeli, hii ndiyo sikukuu ya Krismas ambayo kuanzia leo kupitia wakati huu wa majilio; tunajiandaa kwa kila namna: kiroho na kimwili kwa hali na mali kuisherekea. Mungu anakuwa mwanadamu na mwanadamu anapewa hadhi ya kuwa mwana wa Mungu.

Kwa kipindi cha Majilio, leo Kanisa linatupigia mbiu kupitia Yohane Mbatizaji likisema: «Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia: hii ni sauti ya mtu aliaye nyikani, itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake!» (Matayo 3: 2-3). Majilio ni mbiu na kipindi kiliturujia kinacho tualika tujiandae kumpokea Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kwa upendo wake katika historia anakubali kutwaa mwili yaani kuwa mtu na kuja kuishi na kukaa kati yetu kama wanadamu pasipo dhambi, ili aweze kutukomboa.

Yatupasa daima kukumbuka kuwa, yeye ni «Mungu pamoja nasi» yaani «Emanueli» na mara nyingi anakuja kwetu katika matukio matatu muhimu: Krismas, kifo chetu na ule wakati wa hukumu ya mwisho. Lakini Yesu anakutana na mwamini kwa njia ya Neno, Sakramenti, Maskini na kwa njia ya Matendo ya Huruma. Kipindi hiki cha Majilio, kithimize kutangaza Injili ya Kristo kwa furaha zaidi kama anavyohimza Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, Furaha ya Injili.

Padre Simon Masondole
Jimbo Katoliki Bunda.








All the contents on this site are copyrighted ©.