Ijue Liturujia ya Kanisa tayari kujimwaga kisawasawa kutangaza Injili ya Furaha
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha tafakari ya kina inayoletwa
kwako na Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara ambaye pia ni
Mwenyekiti Idara ya Liturujia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuhusu Liturujia
na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa, wakati huu bado Kanisa linapoendelea
kutafakari yaliyojiri kwenye Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican, tayari kutweka hadi kilindini ili kutangaza Injili ya Furaha
kwa Watu wa Mataifa.
“‘Maana kwa
njia ya liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi
wetu’. Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waonyeshe katika maisha yao na kuwadhihirishia
wengine fumbo la Kristo na pia maumbile halisi ya kanisa la kweli. Kanisa kwa undani
kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana ndani yake, lenye bidii kubwa
katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye
kuhiji. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu,
yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao
tunakoelekea.
Hivyo Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa
wawe hekalu takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utumilifu
wa Kristo. Wakati huohuo kwa namna ya ajabu Liturujia inaimarisha nguvu za waamini
kumhubiri Kristo; na kwa njia hiyo inawaonyesha wale walio nje (nalo) Kanisa lililo
ishara iliyoinuliwa juu kati ya mataifa, ambayo chini yake watoto wa Mungu waliotawanyika
wakusanyika katika umoja, mpaka liwapo zizi moja na mchungaji mmoja (SC 2).
Asili
ya neno liturujia ni maneno mawili ya kigiriki Laos = watu ergon = kazi.
Hivyo neno hilo lilikuwa likitumika kuonyesha
kazi zifanywazo
na watu kwa faida yao wenyewe. Mf. Kuchimba kisima, kujenga shule, n.k. Kazi zilizofanywa
na mtu mmoja kwa faida ya jumuiya nzima, hasa katika uwanja wa elimu, maburudisho,
ulinzi. Kazi zilizofanywa na watumwa kwa bwana wao.
Lakini Biblia
ya Kigiriki (OT) ilitumia neno liturujia kumaanisha:
Kumtukuza
Mungu. Tuseme kwa ujumla mambo ya ibada.
Katika Agano Jipya limetumika
mara 15 kumaanisha
Makuhani (mf. Zakaria Lk. 1:23), Walawi na huduma
yao, Sadaka ya Kristo Wakristo hufanya liturujia, n.k.
Katika
mafundisho / maandishi ya Kanisa Kadiri ya Mediator Dei iliyotolewa
na Papa Pius XII, Nov. 20, 1947.
Ni adhimisho la hadhara ambamo, Kristo
Mkombozi wetu anamtukuza Mungu Baba; pia ni adhimisho la hadhara ambamo Kanisa linamtukuza
Kristo, mwanzilishi wake; na kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake, Kanisa linamtukuza
Mungu Baba. Kifupi ni tendo la kumtukuza Mungu lifanywalo na Mwili wote wa fumbo,
yaani Kichwa na mwili.
Hivyo:
Liturujia ya Kanisa ni mwendelezo
wa liturujia ya Kristo (SC 5: Maana, kutoka ubavuni mwa Kristo akilala msalabani ilitoka
sakramenti ya ajabu ya Kanisa lote) Liturujia ya Kanisa ni ya Kanisa zima, Mapadre
na Walei (SC 14: Mungu “ambaye hutaka watu wote waokolewe …) Katika liturujia,
Kristo ni njia ya lengo la liturujia.
Kadiri
ya Sacrosanctum Concilium (Des. 4, 1963)
Ni utekelezaji wa kazi ya
kikuhani ya Yesu Kristo. Katika Liturujia, kwa ishara zinazoonekana, huonyeshwa na
kutendeka kutakatifuzwa kwake binadamu, kila ishara ikiwa na maana ya pekee. Katika
Liturujia, ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa fumbo wa Yesu Kristo,
yaani na Kichwa na viungo vyake. Kwa hiyo kila adhimisho la kiliturujia, kwa kuwa
ni tendo la Yesu Kristo Kuhani na la Mwili wake, ndilo Kanisa, ni tendo takatifu kupita
yote na hakuna tendo jingine la Kanisa linalofanana nalo kwa manufaa kwa kiwango kile
kile na kwa daraja ile ile (SC 7).
Hivyo:
Liturujia ni
utekelezaji wa kazi ya kikuhani ya Yesu Kristo (SC 2, 5, 6, 8-11, 14, 21, 32, 41 na
43). Liturujia ni tendo la kuabudu linalofanywa na Kanisa zima (SC 7, 14). Liturujia
hufanywa kwa njia ya alama (SC 7) Liturujia ni chemchemi na kilele cha shughuli
zote za Kanisa (SC 7, 10)
Asili ya liturujia ya Kanisa
Mtaguso
wa II wa Vatican unaeleza kuwa liturujia, ambayo yaweza pia kuelezwa kuwa ni mkutano
kati ya mtu na Mungu katika Kristo, ndani ya Kanisa katika alama takatifu, ni tendo
la hali ya juu sana, na hasa ni kilele cha maisha ya ukristo. Katika kusherehekea
mafumbo ya liturujia tunamtukuza Mungu kadiri Mungu mwenyewe anavyotaka. Hivyo inaweza
kuelezwa kuwa liturujia:
Mungu Baba (Liturgy is Theocentric):
Kiini
cha liturujia ni Mungu mwenyewe Mkutano huo kati ya Mungu na mtu ni mkutano kati
ya pande mbili zisizo sawa. Ni kati ya Muumba na kiumbe; kati ya Mungu mkamilifu na
mtu ambaye anamtegemea Mungu kwa kila kitu. Mungu ndiye anayeanzisha / anayeitisha
mkutano huo.
Lengo la liturujia ni utukufu kwa Mungu. Maisha ya binadamu lazima
yaelekezwe kumjua Muumba wake. Agano kati ya Mungu na Mwanadamu ni kati ya pande zisizo
sawa: Udogo huu wa binadamu mbele ya Mungu huonyeshwa kwa namna binadamu anavyotakiwa
kujinyenyekesha mbele ya Mungu kwa kumsifu, kumwomba, n.k.
Mungu Mwana ametukomboa: Katika
liturujia tunakutana na Mungu Baba kwa njia ya Yesu Kristo katika Roho Mtakatifu.
Kristo yupo katika maadhimisho ya liturujia yetu kwa namna mbali mbali: Katika Neno
lake, Sakramenti, Mwili na Damu, Watumishi na mkutano wa kidini. Kwa namna ya pekee,
kwa fumbo la Pasaka Kristo anatupatanisha tena ulimwengu na Mungu. Rejea: Worship
in time and space.
Roho Mtakatifu: Hakuna awezaye kusema kuwa Kristo ni
Bwana ila kwa nguvu ya Roho Mtakatifu (IKor 12:3). Ndiye anayetufundisha na kutukumbusha
yote aliyosema Kristo (Yoh 14:26). Kwa leo tunatia nanga sehemu hii ya kwanza ya tafakari
kuhusu maana ya Liturujia kama inavyochambuliwa kwako na Askofu Salutaris Melchior
Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara na Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania.