Changamoto za kumtangaza Kristo katika nyakati za dijitali!
Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei litaanza mkutano wake wa ishirini na sita wa mwaka
hapo tarehe 5 hadi 7 Desemba 2013, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Kumtangaza Kristo
katika nyakati za Dijitali". Kwa mada hii, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuendeleza
changamoto za Uinjilishaji katika ulimwengu wa mitandao, dhana iliyoanzishwa na Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.
Katika kipindi cha miaka kumi
iliyopita, Kanisa limeendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika njia za mawasiliano
ya kijamii kama jukwaa linalopaswa kusaidia mchakato wa Uinjilishaji, lakini pia njia
hizi zinapaswa kuinjilishwa. Wajumbme watapata fursa ya kupanga na kupitisha mikakati
ya kichungaji itakayotekelezwa na Baraza hili kwa siku za usoni.
Baraza la
Kipapa kwa ajili ya walei linasema, kwamba, waamini walei ni wadau wakuu katika matumizi
ya njia za mawasiliano ya kijamii. Wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba,
wanachangia kikamilifu katika Kuinjilisha mitandao ya kijamii kadiri ya mpango wa
Mungu na kama sehemu ya binadamu kuweza kukutana na Yesu Mkombozi wa dunia. Waamini
walei wanapaswa kutambua changamoto kubwa iliyoko mbele yao kutokana na maendeleo
ya sayansi na teknolojia ya habari.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka
wake wa Kitume, Injili ya Furaha, Evangelii Gaudium anawataka waamini na watu wote
wenye mapenzi mema kutambua dhamana na wajibu wa Kanisa kwamba, ni la Kimissionari
na linatumwa kwenda kutangaza Kweli za Kiinjili hadi miisho ya dunia. Njia ya mawasiliano
ni nyenzo muhimu sana katika utekelezaji wa dhamana na utume wa Kanisa na kwamba,
watu wanahitaji kusikia na kuonja ile Injili ya Furaha.
Wawezeshaji waliochaguliwa
kushiriki katika mkutano wa ishirini na sita ni watu wenye weledi, uzoefu na mang'amuzi
makubwa katika masuala ya mitandao ya kijamii. Wajumbe wataangalia fursa, changamoto
na matatizo yanayojitokeza kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii hasa miongoni
mwa vijana wa kizazi kipya. Licha ya magumu yote haya, lakini Kanisa halina budi kuwa
mstari wa mbele katika matumizi ya mitandao ya kijamii kama jukwaa la kutangaza INJILI
YA FURAHA.
Baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni pamoja na: Utangazaji wa Habari
Njema ya Wokovu katika Ulimwengu wa utandawazi; dunia ya mitandao, muundo wa kisaikolojia
na utambulisho wa watu. Kwa hakika, wajumbe wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei
linataka kuzama zaidi katika matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kama jukwaa la
Uinjilishaji Mpya.