2013-11-29 09:06:51

Marehemu Askofu John Andrea Simalenga azikwa kwa heshima kubwa mjini Njombe!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameongoza mamia ya watu kwenye ibada ya mazishi ya Askofu wa Saba wa Dayosisi ya South West Tanganyika ya
Kanisa la Anglikana Tanzania Mhashamu Askofu John Andrea Simalenga
iliyofanyika Njombe mjini.
Akizungumza na mamia ya waumini na waombolezaji waliohudhuria ibada hiyo ya mazishi Alhamisi, Novemba 28, 2013 Waziri Mkuu alisema Dayosisi hiyo imepoteza mhimili muhimu lakini akawataka wawe na umoja na upendo huku wakiendelea kumtumainia Mungu.

“Mhashamu Baba Askofu Simalenga alisimikwa Julai 6, 2008. Ni miaka
mitano tu ya utumishi kwenu na alikuja wakati ambapo Dayosisi hi ilikuwa imekaa kwa miaka 10 bila ya kuwa na kiongozi. Siku anawekwa wakfu nilikuwepo na ninakumbuka mlimuomba asaidie kuleta mshikamano,” alisema Waziri Mkuu. “Ninawaomba wanadayosisi muwe na upendo na mshikamano mkubwa miongoni mwenu hadi hapo Mungu atakapotupatia kiongozi mwingine. Tumuombe Mungu ili kiongozi huyu ajaye apatikane kwa njia ya amani,” alisisitiza.


Alimwomba mke wa marehemu, Bibi Martha pamoja na watoto wa marehemu
waupokee msiba huo kwa mikono miwili na kuahidi kuwaombea faraja kwa
Mwenyezi Mungu. Waziri Mkuu ambaye alishiriki mazishi hayo kwa niaba ya Serikali, Alitumia fursa hiyo kuwapa pole maaskofu, mapadre, watawa na familia
zikiwa ni salamu maalum kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alisema
yuko ziarani kwenye mkoa mpya wa Simiyu.

Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bibi Anne Makinda ambaye pia ni mbunge wa Njombe Kusini ilipo Dayosisi hiyo akitoa salamu za rambirambi alisema wana Njombe wamepungukiwa na nguvu kwa kuondokewa na Askofu Simalenga. “Alisaidia kuleta umoja hapa kwetu, tumempoteza mtu muhimu sana katika harakati za maendeleo ya wilaya yetu na mkoa kwa ujumla. Alisaidia kuleta umoja na upendo na sisi tuwe na upendo na amani, tuendelee kumuomba Mungu hadi tutakapoletewa msimamizi mwingine.
Katika mahubiri yake kwenye ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la
Anglikana Tanzania, Mhashamu Jacob Chimeledya aliwataka waumini wote
wamtazame Mungu na wamtegemee Mungu kwa sababu wanampenda lakini yeye ameona ni vema ampunzishe mtumishi wake.
“Sote tunajua kuwa katika kipindi chake, Dayosisi hii ilitulia kabisa Je, tutaruhusu kuondoka anikwake kuzue tena chokochoko? Msiba huu usifike mahali ukaanza kututenganisha na kutoa mwanya wa kuanza kunyoosheana vidole. Tumuombe Mungu atusaidie afute machozi yetu,” alisema.

Askofu John Andrea Simalenga alizaliwa Novemba 30, 1953 na kufariki
Novemba 24, 2013 baada ya kuugua kwa siku mbili. Novemba 22, 2013 alijisikia vibaya na alipopimwa aliikutwa na malaria, kisukari na shinikizo la damu. Alilazwa hospitali ya Kibena, Njombe na kuruhusiwa siku iliyofuata lakini Novemba 24 alizidiwa tena na kuaga dunia. Ameacha mjane na watoto wanne.








All the contents on this site are copyrighted ©.