Madhulumu ya waamini wa dini ya Kiislam nchini Angola?
Serikali ya Angola imekanusha tetesi kwamba, ilikuwa na mpango wa kufunga misikiti
yote nchini Angola kwa kukosa usajili si za kweli na kwamba, Serikali haina mpango
wa kuwadhulumu wala kuwanyanyasa waamini wa dini ya Kiislam nchini Angola. Ufafanuzi
huu umetolewa na Bwana Manuel Fernando, Mkurugenzi wa taasisi ya kitaifa ya masuala
ya kidini, Wizara ya Utamaduni nchini Angola.
Tetesi kwamba, Serikali ya Angola
inataka kufunga misikiti yote nchini humo kwa vile haikusajiliwa zimepokelewa kwa
hisia tofauti na watetezi wa haki msingi za binadamu, kwani ikiwa kama uamuzi huu
utatekelezwa unaweza kusababisha mtafaruku mkubwa miongoni mwa wananchi wa Angola.
Serikali pia inasemekana kuwa na mpango wa kufuta madhehebu ya Kikristo yasiyosajiliwa
na yale ambayo yanakwenda kinyume cha mila, desturi na tamaduni njema za Angola.
Bi
Rosa Cruz e Silva, Waziri wa habari nchini Angola amenukuliwa na vyombo vya habari
akisema kwamba, Dini ya Kiislam haikupata usajili nchini Angola kadiri ya sheria za
nchi. habari hizi zimechafua hali ya hewa kwa Serikali kushutumiwa kwamba, inaendesha
madhulumu ya kidini dhidi ya waamini wa dini ya Kiislam. Sheria inaonesha kwamba,
ili kikundi cha waamini wa dini yoyote nchini Angola kiweze kuendesha shughuli zake
lazima kwanza kabisa kisajiliwe Serikalini. Ikiwa kama sheria hii itatekelezwa zaidi
ya misikiti 70 itabomolewa!
Takwimu zinaonesha kwamba, Angola ina wananchi
wapatao millioni 19. kati yao kuna: wakristo millioni 17. 2; Waislam 40, 000; 10,
000 Wabudha na Waebrania. Baadhi ya waamini wanashindwa kupata kibali cha Serikali
kutokana na kushindwa kukidhi masharti ya sheria za nchi. Wachunguzi wa mambo wanasema
sheria hii haitekelezeki.