2013-11-29 11:05:08

Hali ya ugonjwa wa Ukimwi Barani Afrika


Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF katika taarifa yake iliyozinduliwa tarehe 29 Novemba 2013 inaonesha kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchakato wa kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2012. Watoto 850, 000 wamekingwa dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, lakini hali inatisha miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto yamepungua kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha Mwaka 2009 hadi mwaka 2012: Ghana kwa 76%, Namibia 58%, Zimbabwe 55%, Malawi 52%, Botswana 52%, Zambia na Ethiopia ni 50%. Wanawake walioathirika kwa virusi vya Ukimwi kwa asilimia 60 kutoka katika nchi zinazoendelea wamepata huduma ya afya ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto.

Kwa mwaka 2012 ni watoto 34% tu waliobahatika kupata dawa za kurefusha maisha, ikilinganishwa na asilimia 63% ya watu wazima. Inakadiriwa kwamba, katika kipindi hiki watoto 210,000 wamefariki kutokana na Ukimwi pamoja na magonjwa mengine nyemelezi. Kuna watoto ambao wanaishi na virusi vya Ukimwi bila kupata tiba na wanatarajiwa kufariki dunia katika kipindi cha miaka miwili, ikiwa kama juhhudi za makusudi hazitafanyika kuwapatia dawa za kurefusha maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.