Baba Mtakatifu Francisko anapania kuwaimarisha wanafunzi katika azma ya Uinjilishaji
Mpya
Zaidi ya wanafunzi 10,000 kutoka katika Vyuo Vikuu na Taasisi za elimu ya juu zilizoko
mjini Roma wanatarajiwa kushiriki katika Ibada ya Masifu ya kwanza ya Kipindi cha
Majilio, yatakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, majira ya jioni kuanzia
saa 11:30 kwa saa za Ulaya. Haya ni Mapokeo kwa Baba Mtakatifu kukutana na wanafunzi
kabla ya Noeli, ili kuwaandaa vyema zaidi katika kipindi cha Majilio.
Kama
sehemu ya maandalizi haya, Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la
Roma atapokea Sanamu ya Bikira Maria Kikao cha Hekima na kuongoza tafakari ya Rozari
takatifu, muhtasari wa Injili.
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Sanamu
ya Bikira Maria Kikao cha Hekima, ilitunzwa na wanafunzi kutoka Brazil kama sehemu
ya ushiriki wao kwa Maadhimisho ya Siku ya Vijana iliyofanyika Mwezi Julai, 2013,
mjini Rio de Janeiro, Brazil. Mwaka huu, Wanafunzi kutoka Ufaransa ndio watakaokaabidhiwa
Sanamu hii tayari kuitembeleza kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini
Ufaransa.
Wakati huo huo, Askofu Lorenzo Leuzzi anatarajia siku ya Ijumaa usiku
kuongoza Ibada ya Misa takatifu kwenye Chuo Kikuu cha Tor Vergata. Ibada ya Masifu
ya Jioni itakaoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko ni tukio muhimu sana kwa wanafunzi
wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, kwani Baba Mtakatifu anapenda kuitumia fursa
hii kuwahimiza wanafunzi kuwa wadau wakuu wa Uinjilishaji miongoni mwa wanafunzi wenzao
katika Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu