Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewataka maafisa mipango miji nchini kurekebisha
utendaji wao wa kazi ili waweze kubadili taswira mbaya iliyojengeka miongoni mwa jamii
dhidi yao. Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Novemba 27, 2013, wakati akifungua Mkutano
wa Kwanza wa Wataalam wa Mipangomiji waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wataalam
wa Mipangomiji ulioanza leo jijini Dar es Salaam. “Taswira ya utendaji kazi katika
taaluma ya mipangomiji na katika sekta ya ardhi kwa ujumla miongoni mwa wananchi
na Serikali siyo nzuri sana. Watafiti wanatueleza kuwa kati ya asilimia 60 na 80 ya
makazi kwenye miji yetu hapa nchini yamejengwa kiholela. Na kwa kiwango hicho hicho
wakazi wa mijini wako kwenye makazi hayo na wanaishi kiholela,” alisema. “Wako
wanaosema ninyi ndiyo chanzo cha hiyo migogoro, wako wanaosema ninyi kwa rushwa ndiyo
wenyewe, mimi sishangai madai haya ila ninawasihi muwe na roho ngumu katika kushinda
vishawishi hivi,” alisisitiza. Aliwataka wajadili masuala yanayohusu migogoro ya
ardhi bainaya wafugaji na wakulima, baina ya mipaka ya vijiji, baina ya wilaya, baina
ya wanavijiji na hifadhi za Taifa au maeneo ya uchumbaji madini na kujadili njia za
kutatua migogoro hiyo ili kuwa na mipamgo endelevu. Aliwataka waangalie suala
la ukuaji wa miji iliyokaribu na Jiji la Dar es Salaam kwa kuangalia dhana ya miji
mikubwa kubeba vijiji vinavyoizunguka na hasa kuangalia uwezekano wa kupunguza mlundikano
wa watu katika jiji hilo. “Miji ya Kibaha, Mkuranga na Bagamoyo inatumikaje kusaidia
kupunguza msongamnano katika jiji la Dar es Salaam,” Waziri Mkuu alihoji Alisema
wataalamu wa mipango miji wanapaswa kuwa na maono makubwa ya baadaye kama kweli wanataka
kupunguza majanga katika siku za usoni. “Angalieni utafiti wa gesi unaoendelea pale
Mtwara na mjipange, angalieni mpango wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na kuunganisha
na reli ya kati, angalieni Lindi na upatikanaji wa Liquified Natural Gas (LNG), pangeni
miji kwa siku za baadaye siyo sasa,” alisisitiza. Aliwataka wanataaluma hao wasimamie
vema taaluma yao kwani katika miaka 37 ijayo, (mwaka 2050) inakadiriwa kwamba nusu
ya watu wote watakuwa wakiishi mijini. “Kuweni wakweli, tumieni weledi wenu la sivyo
katika miaka 37 ijayo kama wanavyosema watafiti, itakuwa balaa tupu,” alisema.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wataalamu hao kutoka mikoa yote hapa
nchini, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka alisema maafisa
mipango miji wanakabiliwa na changamoto ya kufikiri na kubuni aina ya miji ambayo
itakidhi mahitaji ya jamii ya baadaye.
Alisema hata hivyo maafisa hao wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto ya kushindwa kutoa maamuzi ama ushauri wa kitaalamu kwa
kuhofia kuadhibiwa na madiwani.