2013-11-27 09:10:05

Kongamano la kimataifa kuhusu uchumi mshikamano na maendeleo kwa Bara la Afrika kufanyika tarehe 29 Novemba 2013 mjini Vatican


Baraza la Kipapa la Taasisi za Sayansi kwa kushirikiana na Mfuko wa "Sorella Natura", tarehe 29 Novemba 2013 litaendesha Kongamano la Kimataifa kuhusu uchumi mshikamano na maendeleo kwa Bara la Afrika. Tarehe 29 Novemba 2013 ni siku ambayo ina umuhimu wake wa pekee, kwani ni ile siku ambayo Mtakatifu Francisko wa Assisi alitangazwa kuwa ni msimamizi wa watunza mazingira.

Kongamano hili linapania pamoja na mambo mengine kuvuta hisia za wadau mbali mbali ili waweze kuona umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutafuta ufumbuzi wa kudumu kwa matatizo na changamoto zinazolikabili Bara la Afrika, kwa kujikita zaidi katika masuala ya uchumi mshikamano unaoweza kusaidia kukoleza maendeleo endelevu Barani Afrika.

Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa haina budi kuanza kuwa na mwelekeo mpana zaidi badala ya kujikita katika utoaji wa misaada ya kujikimu kwa nchi za Kiafrika na kuanza kuwekeza katika miradi mikubwa inayopania ustawi na maendeleo ya wananchi wa Bara la Afrika. Hatari ni kwamba, Bara la Afrika limeendelea kunyonywa katika mifumo mbali mbali ya kiuchumi, hata leo hii kuna ukoloni mamboleo ambao umekuwa ni kikwazo kikubwa cha ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika.

Bara la Afrika linachangamotishwa na wapenda haki na amani kuhakikisha kwamba, watu wake wanasimama kidete kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao na ustawi wa wananchi wa Bara la Afrika. Wananchi na wapenda maendeleo washirikishwe kikamilifu katika mikakati ya kukabiliana na changamoto za maisha Barani Afrika.

Kati ya wazungumzaji wakuu kwenye Kongamano hili ni Kardinali Monsengo Pasinya, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC. Wakati wa kongamano hili, Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Caritas Internationalis, Professa Romani Prodi Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Ukanda wa Sahel pamoja na Professa Paolo Scaroni. Viongozi hawa watapewa Shahada ya Udaktari wa heshima kutoka katika Chuo Kikuu cha Burkina Faso kutokana na mchango wao mkubwa kwa maendeleo na ustawi wa Bara la Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.