2013-11-27 15:22:59

Kalenda ya maadhimisho ya Papa Francisko kwa Desemba na Januari


Jumanne, Ofisi ya Liturujia ya Kipapa , ilitangaza mtiririko wa Maadhimisho ya kiliturujia yatakayo ongozwa na Papa Francisko katika kuukamilisha mwaka 2013 na mapokezi ya mwaka mpya Januari 2014.
Tukio la kwanza, litakuwa Jumamosi tarehe 30 Novemba, katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, majira ya 11:30 za jioni, Papa atakutana na wanafunzi wa Vyuo Vikuu Jimboni Roma, ambamo ataongoza sala ya masifu ya jioni , kwa nia ya kuzindua kipindi cha Majilio.
Siku ya Jumapili Mosi Desemba, Papa atafanya ziara ya kichungaji katika parokia ya Mtakatifu Cyril Alexandrino ya Rome, majira ya saa kumi na mbili ambako ataongoza Ibada ya Misa.
Na tarehe 8 Desemba, Papa atakwenda katika uwanja wa Spagna jijini Roma, ambako kuna Madhabahu ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, kutoa heshima zake kwa Maria kama ulivyo utamaduni wa Mapapa kwa kila mwaka.
Na kwa ajili ya maadhimisho ya kilele cha Noel, Desemba 24, Papa ataongoza Ibada ya Misa ya Noel majira ya saa tatu na nusu za usiku katika Kanisa Kuu la Mtaktifu Petro Vatican , na kesho yake 25 majira ya mchana ataota baraka zake za "Urbi et Oribi" tokea makazi yake ya kipapa hapa Vatican.
Papa atakamilisha mwaka 2013 kwa kuongoza Ibada ya Shukurani kwa Mungu "Te Deum", majira ya saa kumi na moja za jioni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.

Januari 1, 2014, saa 4:00 asubuhi , ataongoza Ibada ya Misa kwa ajili ya Siku Kuu ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na ambamo pia itakuwa ni Siku ya Amani Duniani ya 47.
Jumatatu, Januari 6 ambayo ni Sikukuu ya Epifania, Papa Francisko, ataongoza Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro majira ya saa nne za asubuhi,
Jumapili ya 12 Januari, Papa ataongoza Ibada kwa ajili ya kutoa Sakramenti ya ubatizo kwa watoto kadhaa, katika kanisa Sistine la ndani ya Vatican majira ya saa 3:45za asubuhi.









All the contents on this site are copyrighted ©.