Watu wanaonesha imani, ukarimu na mshikamano wa dhati licha ya majanga yanayowakabili
Licha ya taabu na magumu ambayo wananchi wa Ufilippini wanakabiliana nayo kwa sasa,
lakini bado ni watu wenye imani, ukarimu na mshikakano wa dhati kati yao. Hayo yamesemwa
na Monsinyo Paul Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii ambaye
kwa sasa yuko nchini Ufilippini kuhudhuria Kongamano la pili la Vyombo vya mawasiliano
ya Jamii nchini Ufilippini.
Monsinyo Tighe anasema kwamba, vyombo vya habari
vimekuwa mstari wa mbele kuhabarisha yale yaliyokuwa yanajiri nchini Ufilippini baada
ya kukumbwa na tufani kali, iliyosababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu pamoja
na miundo mbinu kiasi kwamba, watu wengi bado wanahitaji msaada wa dharura ili kukabiliana
na majanga haya! Mawasiliano haya yamewagusa wengi na watu wakajitoa kuonesha mshikamano
wao a dhati, kama walivyofanya waamini wakati wa kufunga Mwaka wa Imani kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Novemba 2013.
Vatican
kwa njia ya mashirika yake ya misaada kitaifa na kimataifa inaendelea kuwahamasisha
waamini na watu wenye mapenzi mema kuchangia kwa hali na mali katika harakati za kuwasaidia
waathirika wa tufani nchini Ufilippini. Huu ndio mwelekeo wa ujumla kwa waamini kutoka
Majimbo na Parokia mbali mbali duniani. Mwaka wa Imani imekuwa ni fursa ya kujenga
na kuimarisha mshikamano wa upendo kati ya watu!
Monsinyo Tighe anasema, kuna
haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatumia kikamilifu maendeleo ya sayansi
na teknolojia ya habari kwa ajili ya kutangaza kweli za Kiinjili. Ili kufanikisha
azma hii kuna haja ya kufahamu lugha ya wale watu wanaoishi kwenye ulimwengu wa mitandao.
Mambo makuu matatu ya kuzingatiwa ni: kuzungumza, kushirikishana na kujadiliana. Watu
wanaoishi katika ulimwengu wa mitandao wasaidiwe kujenga utamaduni wa majadiliano
na kujitahidi kuishi kadiri ya tunu msingi za Kiinjili.