Rais Putin akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni tarehe 25 Novemba 2013 amekutana na kuzungumza
na Rais Vladimir Putin wa Russia. Baadaye Rais Putin na ujumbe wake walikutana na
kuzungumza na Askofu mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyeambatana na
Askofu mkuu Dominique Mamberti, katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican.
Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wameelezea
kuridhishwa kwao na uhusiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na baadaye, walijadili
mambo yanayogusa mafao ya pande hizi mbili, hususan maisha ya Waamini wa Kanisa Katoliki
nchini Russia na mchango wa Wakristo katika ustawi na maendeleo ya Russia. Wamejadili
pia hali ngumu inayowakabili Wakristo sehemu mbali mbali za dunia; umuhimu na kusimama
kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; uhai sanjari na tunu msingi za
maisha ya kifamilia.
Viongozi hawa kwa namna ya pekee kabisa wamejadili kuhusu
mchakato wa amani Mashariki ya Kati na hali tete nchini Syria. Rais Putin amemshukuru
Baba Mtakatifu Francisko kwa barua kwa wakuu wa G20 wakati wa mkutano wao uliofanyika
mjini Pitsburg. Wamekubaliana kimsingi kusitisha vita, kuendelea kutoa huduma na misaada
ya kiutu kwa waathirika pamoja na kukazia majadiliano yanayolenga upatikanaji wa suluhu
ya kudumu nchini Syria. Majadiliano haya yawahusishe wadau mbali mbali ili amani ya
kweli iweze kupatikana.