2013-11-26 15:50:56

Papa Francisko atoa waraka wake wa kitume wa kwanza, juu ya Furaha ya Injili " Evangelii Gaudium".


Baba Mtakatifu Franciisko Jumanne hii ametoa waraka wake wa Kwanza wa Kitume chini ya Jina Furaha ya Injili “Evangelii Gaudium". Waraka unao zungumzia zaidi juu ya Mada ya utangazaji wa Injili katika Dunia ya nyakati hizi. Waraka huu wenye kurasa 224, unaonyesha muono wa Papa, katika utume wa Kanisa, ambalo milango yake inapaswa kuwa wazi nyakati zote na kwa watu wote.

Katika waraka huu,Papa amezungumzia mada mbalimbali juu ya Uinjilishaji mpya, masuala ya kijamii kama haki na amani, familia na heshima katika viumbe, imani na siasa, uekumene , majadiliano ya kidini na wajibu wa wanawake na walei katika Kanisa.
Katika maelezo yake, Papa amefanya nukuu kutoka vyanzo vingine vya maelezo, ikiwemo michango ya kazi za Sinodi iliyofanyika Vatican tangu tarehe 7-28 OKtoba 2012 , juu ya mada:Uinjilishaji Mpya kwa ajili ya kuieneza Imani.

Katika waraka hu, Papa Francisko, anawahimiza Waamini wote kujihusisha na utendaji mpya wa kufikisha habari ya upendo wa Kristu kwa watu wote, huku wakiwa wamejawa na moyo wa furaha, katika kuionyesha njia ya hija ya kanisa katika miaka ijayo. Huu ni wito kwa wabatizwa wote kuupeleka upendo wa Kristu, kwa watu wengine, kama utendaji wa kudumu na ushindi mkuu katika dunia ya leo , ambayo imemezwa na ubinafsi, kukata tamaa na mahangaiko ya kidunia.

Papa anawaalika wasomaji wote kungudua upya asili ya Injili , kupata nafasi mpya na njia mpya katika ubUnufu bila ya kumpoteza Yesu katika katika utendaji wote wa kila siku. Katika hili Papa anasema kuna haja ya kuwa na uongofu wa kichungaji na kimisionari , ambao hauwezi kuacha kujali hali zilivyo, na katika kuleta upya kwenye mifumo ya kanisa, ili kuwezesha kanisa, kuwa la kimisonari zaidi.

Papa pia anafikiria uongofu wa utawala katika kiti cha Papa , kwa ajili ya kuwezessha kazi zake kuwa na uaminifu zaidi katika maana ambayo Yesu Kristo alipenda iwe hivyo katika hitaji la kuifikisha habari njema kwa mataifa yote. Anatumaini Mabaraza ya Maaskofu yanaweza kutoa mchango thabiti katika ufanikishaji wa moyo wa umoja na mshikamano wa waamini wote wa Kristu, katika kuitangaza Injili, jambo ambalo anasema bado halijatimizwa kikamilifu.

Pia anasema, kuna umuhimu wa kupeleka mamlaka majimboni. Na kwamba juhudi za mabadiliko haya,Kanisa lisiwe na woga, hasa katika kuchunguza upya baadhi ya kanuni, ambazo hazina mahusiano ya moja kwa moja na kiini cha Imani na Injili, hata kama yana mzizi wa historia ya siku nyingi katika kanisa.

Na akitazama nje zaidi ya Kanisa , Papa ameutazama mfumo wa sasa wa kiuchumi akisema kimsingi ndani mwake hakuna haki,ila ndani mwake mmefichika makucha ya soko la dhuluma, ambamo mna uroho wa fedha ,wenye kueneza rushwa na ukwepaji wa kulipa kodi. Pia Papa anakemea mashambulizi dhidi ya uhuru wa dini na mateso mpya yanayo elekezwa zaidi dhidi ya Wakristo. Na Papa pia anakemea ulimwengushaji wa maadili wenye kuzalisha hisia zinazo wachanganya watu na kuwaweka katika za mashaka, hofu na purukushani. Pia waraka unataja umuhimu wa ndoa na mahusiano ya familia imara.

Papa hakuwasahau watu maskini akisema, umaskini mbaya zaidi ni umaskini wa kiroho. Hata hivyo akahimiza hoja ya kuwajali pia wale wanaoteseka kimwili kutokana na kusahaulika pembezoni mwa jamii kw sabau mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa makazi, na hasa unao sababishwa na uwepo wa machafuko ya mpigano yenye kuzalisha wakimbizi au utendaji wa kiuchumi unaowaondoa watu wenyeji katika makazi yao. Pia ameyataja makundi ya wazee, wahamiaji, waathirika wa biashara na watoto wasiozaliwa bado, ambao hutupwa mitaani.

Hati mpya ya Papa pia inalenga katika mandhari ya kukuza amani, haki na udugu , kwa njia ya majadiliano na mazungumzo ya kuheshimiana watu wote iwe kijamii au kitamaduni na kidini. Pia amehimiza mahusiano mazuri na wakristo wengine, na Wayahudi na Waislamu wote, kama njia muhimu ya kukuza amani na kupambana na ubabe wa kutumia dini kushambulia wngine au kunyima uhuru wa dhamiri kwa wengine.

Amewataka Wakristo kujiepusha na ujenzi wa chuki za ujumla hasa kuhusu Uislamu ,Katika hili, Papa amehimiza Wakristu kuendelea kuwa wanyenyekevu, hasa na nchi za Kiislamu, wakati wanapodai uhuru kamili wa kidini kwa Wakristo.
Waraka umekamilika na sala kwa Mama Bikira Maria , Mama wa Uinjilishaji , akiutazama mfano wa Maria katika kazi za Kanisa za Uinjilishaji, kwamba, tunapomtafakari Maria , kwa mara nyingine hutuwezesha kuamini katika ufunuo asilia wa asili ya upendo na huruma.









All the contents on this site are copyrighted ©.