Msivumishe habari zisizo na msingi katika hali tete kama Nigeria!
Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria anasema, hana
uhakika na uvumi uliosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari ndani na nje ya Nigeria
kuhusu wanawake wa Kikristo kutekwa nyara na kulazimishwa kuolewa na wanajeshi wa
Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram. Anakiri kwamba, wanawake kutekwa na kubakwa ni
vitendo vinavyoendelea nchini Nigeria, hali inayodhalilisha utu na heshima ya wanawake.
Kardinali
Onaiyekan anasema hajui kama kuna kampeni ya kuwakamata wanawake wa Kikristo na kuwalazimisha
kuolewa na wanajeshi wa Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram. Inasikitisha kusikia watu
wakisambaza habari za uvumi na uchochezi katika mazingira kama ya Nigeria ambako hali
ni tete kutokana na madhulumu ya kidini dhidi ya Wakristo. Anawataka waandishi wa
habari kusema ukweli badala ya kutunga habari zinazoweza kusababisha mtafaruku ndani
ya Jamii.
Kardinali Onaiyekan anasema, hivi karibuni, Kikundi cha Kigaidi cha
Boko Haram kimepata pigo kubwa kutoka kwa Jeshi la Serikali, katika Mikoa ya Kaskazini
mwa Nigeria. Kikundi hiki kinaanza kupoteza mwelekeo na dira yake, si kama ilivyokuwa
miezi kadhaa iliyopita.
Lakini anasema Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan,
hii haimaanishi kwamba, Boko Haram imesambaratishwa, bali bado kuna vitendo vya ujambazi
vinavyofanywa na makundi ya Askari na wala si Jeshi la Msituni kama Boko Haram ilivyokuwa
mwanzoni.