Kiasi cha dolla millioni 1 kugharimia miradi ya maendeleo kwa Kanisa Barani Afrika
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani katika mkutano wao wa mwaka uliohitimishwa hivi
karibuni mjini Bartimore, umepitisha kiasi cha dolla za kimarekani 948, 195 zitakazogharimia
miradi 38 inayolenga: majiundo ya shughuli za kichungaji; haki na amani: uongozi na
gharama za uendeshaji. DRC ni kati ya nchi ambazo zitafaidika zaidi na msaada huu
kutokana na kuathirika kwa vita ambayo imekuwa ni chanzo cha majanga mengi nchini
humo.
Majimbo mengi Barani Afrika yameanza kuonesha cheche za kujitegemea
kumbe, msaada unaotolewa ni kwa ajili ya maboresho ya miundo mbinu na majiundo endelevu
anasema Kardinali Theodore McCarrick, Mwenyekiti wa Tume Ndogo ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Marekani kwa ajili ya Kanisa Barani Afrika.
Burkina Faso itasaidiwa
katika maboresho ya njia za mtandao, madarasa na majiundo makini kwa ajili ya walimu,
ambao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu. Shule ni mahali ambapo wanafunzi
wamebahatika kurithishwa imani, maadili na utu wema. Msaada huu unapania kuliwezesha
Kanisa Barani Afrika kujikita zaidi na zaidi katika elimu, kama njia ya kuwaonjesha
wengine ile Furaha ya Injili.