Rais Jakaya Mrisho Kikwete Jumatatu tarehe 25 Novemba 2013 amefanya mazungumzo na
Bibi Mary Robinson, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) katika eneo
la Maziwa Makuu. Mazungumzo baina ya Rais Kikwete na Bibi Robinson yamehusu maendeleo
na hatua iliyofikiwa katika mgogoro wa Mashariki mwa DRC - Congo na jitihada zinazofanywa
za kutekeleza mkataba wa amani ambapo Tanzania imetoa mchango mkubwa katika jitihada
hizo. "Nakupongeza kwa juhudi zako katika masuala ya amani katika nchi za Maziwa
Makuu na pia nakuomba uendelee kutoa mchango wako zaidi wa mambo gani muhimu ya kuzingatia
baadaye”. Bibi Robinson pia amempa salamu za rambirambi Rais Kikwete pamoja na familia
za wanajeshi waliopoteza maisha yao katika harakati za kuleta amani huko mashariki
mwa DRC Congo.
Bibi Robinson amemwomba Rais Kikwete aendelee kutoa mchango
wake kwenye juhudi za kuleta amani nchini Congo baada ya kikosi cha UN kufanikiwa
kuwaondoa waasi wa kikundi cha M23 kutoka Mashariki mwa DRC – Congo. Viongozi hawa
wamekubaliana kuwa ipo haja ya kuendeleza juhudi za kuleta amani DRC na kuangalia
jinsi ya kusonga mbele na kubainisha mahitaji na hatua zaidi za kuchukua katika kuhakikisha
amani na usalama vinapatikana na hatimaye kujenga uchumi wa DRC.
Wakati huo
huo Rais Kikwete amekutana na Rais Mstaafu wa Msumbiji Mheshimiwa Joachim Chissano
ambaye ni msuluhishi wa mgogoro wa Mpaka Kati ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa.
Rais Chissano na ujumbe wake upo nchini kusikiliza hoja za Tanzania kuhusu mpaka wa
Ziwa Nyasa ambapo Rais Kikwete amewasilisha hoja zake kwao. Tayari msuluhishi huyo
ameshasikiliza hoja za Malawi ambapo inatarajiwa hoja za nchi zote mbili hizi zitatafsiriwa
na kuzingatiwa katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo wa Ziwa Nyasa.