Kongamano la dawa asilia kufanyika Jijini Kampala, Uganda, Julai 2014
Mfuko wa Msamaria Mwema ulioanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, unaoendeshwa
na kusimamiwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wafanyakazi katika
sekta ya afya, Jumatatu tarehe 25 Novemba 2013, unafanya mkutano kuhusu Mradi wa Afrika
unaojulikana kama "Africae Munus", kama njia ya kuunda mtandao wa vyuo vikuu kutoka
Barani Afrika, ili kushirikishana utajiri wa ujuzi, rasilimali, miradi na malengo
mbali mbali mintarafu Mafundisho ya Mababa wa Kanisa.
Mradi huu ulizinduliwa
Mwaka 2012 na kwa sasa unavishirikisha vitivyo vya afya kutoka: DRC, Msumbiji, Chad,
Burkina Faso, Tanzania na Uganda. Mkutano huu pamoja na mambo mengine unachambua mafanikio
yaliyokwisha kupatikana katika kipindi cha mwaka mmoja ili kuweka mikakati inayotakiwa
kutekelezwa kwa siku za usoni. Lengo ni kusaidia kujenga uwezo wa Kanisa Barani Afrika
kuwaandaa mabingwa katika sekta ya afya, kwa kushirikiana na vyuo vikuu Barani Ulaya,
Amerika ya Kusini na Canada.
Mkutano huu unazungumzia pia kongamano la kimataifa
litakalofanyika Jijini Kampala, Uganda, mwishoni mwa Mwezi Julai 2014 ili kujadili
kuhusu Dawa Asilia.