Kanisa Katoliki nchini Kenya imekuwa ni mdau wa maendeleo endelevu ya mwanadamu kiroho
na kimwili katika sekta ya elimu, afya, mawasiliano na maendeleo endelevu ya mwanadamu
katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema
kwamba, liko tayari kuungana na wananchi wa Kenya katika kumwimbia Mungu utenzi wa
sifa na shukrani, Kenya itakapokuwa inaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu ilipojipatia
uhuru wa bendera kutoka kwa Mwingereza. Hayo yamebaianishwa na Padre Vincent Wambugu,
Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya na kwamba, Kanisa daima limewasindikiza
wananchi wa Kenya katika hija ya maisha yao ka takribani miaka hamsini na litaendelea
kufanya hivyo, kuelekea katika maisha ya uzima wa milele. Jubilee ya Miaka 50
ya uhuru wa Kenya iwe ni fursa ya kujiwekea mikakati makini ya kuwahudimia wananchi
wa Kenya kwa ari na moyo mkuu kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Baraza
la Maaskofu Katoliki Kenya limekwisha panga mikakati ya maendeleo kwa kipindi cha
miaka kumi kuanzia sasa na kwamba, huu utakuwa ni mchango muhimu sana katika kutafuta
mafao ya wengi na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Kenya. Kanisa Katoliki Kenya
linamiliki na kuendesha kiasi cha asilimia 30% ya taasisi zote za sekta ya afya nchini
humo. Lina Hospitali 54, Vituo vya Afya 83 na Zahanati 311. Kanisa lina miliki
taasisi za elimu zipatazo 8000; kati ya hizi, kuna shule za msingi 5600, Sekondari
1900, Taasisi za elimu ya juu 5 na Chuo Kikuu kimoja. Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru
wa Kenya itafikia kilele chake kati ya tarehe 11 na 12 Desemba 2013 kwenye Bustan
za Uhuru na Kiwanja cha Karasani. Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
katika Maadhimisho haya.