2013-11-25 08:15:59

Halmashauri walei Jimbo kuu la Dar es Salaam wala kiapo!


Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Kristo Mfalme sanjari na kilele cha Mwaka wa Imani, Askofu msaidizi Titus Mdoe wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, aliendesha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwasimika viongozi wa Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ibada hii imefanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam.

Katika mahubiri yake, Askofu msaidizi Mdoe aliwakumbusha viongozi wa Halmashauri ya Walei dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa; akawataka kuwa mstari wa mbele katika kuonesha dira na mwanga utakaosaidia mchakato wa utekelezaji wa maamuzi mbali mbali yanayofanywa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Askofu msaidizi Mdoe anasema, Yesu Kristo ni Mfalme wa Ukweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, mapendo na amani. Kama viongozi wa Kanisa wametwaliwa kati ya watu kwa ajili ya kusimamia maisha na utume wa Kanisa, changamoto ya kumpenda Mungu na watu wake. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam imewaamini na kuwathamini kwa kuwakabidhi majukumu haya mazito baada ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, mwaliko kwao wa kuwatumikia kwa moyo wa uchaji, unyenyekevu na pasi na makuu.

Amewataka viongozi wa Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar es Salaam kumwiga Kristo aliyejinyenyekesha hata akajitwalia hali ya ubinadamu, katika mambo yote akawa sawa na binadamu, lakini hakutenda dhambi; alitii hata kukubali kifo cha Msalaba, kielelezo cha kiongozi makini aliyewapenda watu wake upeo! Alionesha mfano wa uongozi kwa njia ya mifano ya maisha yake, hata wao wanapaswa kuwa kweli ni watumishi wa Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Kamwe wasitake kuwa ni Mabwana na wakandamizaji, kwani uongozi ni safari ya maisha! Wasiwe ni viongozi wa kwanza "kutupa madongo" kwa Maparoko wao, bali kwa unyenyekevu na moyo mkuu wajitafiti kwanza mioyoni mwao ikiwa kweli wametekeleza wajibu wao kama waamini walei na viongozi wa Kanisa.

Askofu msaidizi Titus Mdoe amewataka viongozi Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar es Salaam kuhakikisha kwamba, wanasoma na kutafakari Neno la Mungu, tayari kulimwisha katika uhalisia wa maisha yao, pili wanaifahamu vyema Katekisimu ya Kanisa Katoliki, dira na mwongozo wa maisha yao ya kiroho; tatu, wajitahidi kuyafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa, tayari kushiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Kimsingi Askofu msaidizi Titus Mdoe anasema, ni nyenzo zinazoweza kuwasaidia kutekeleza wajibu wao kama viongozi wa Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar es Salaam.







All the contents on this site are copyrighted ©.