Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya, hivi karibuni amehitimisha
Mwaka wa Imani kwa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki na Kati,
CUEA kwa Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kuwapokea Wakatekumeni wapya kumi na watu
ambao wameanza hija ya maisha ya kiroho, wakitaka kuingia kwenye Mlango wa Imani,
ili hatimaye, wapokee Sakramenti ya Ubatizo. Wakatekumeni hawa ni kutoka katika Jumuiya
ya Chuo Kikuu cha CUEA. Askofu mkuu Balvo amewakabidhi Wakatekumeni wapya Biblia
Takatifu, ili Neno la Mungu liweze kuwaangazia katika mapito ya maisha yao, kwa kujitahidi
kumfahamu Kristo kwa njia ya Maandiko Matakatifu, ili siku moja waweze kumtolea ushuhuda
wa kweli. Wakatekumeni hao wamepewa Msalaba, kielelezo cha Fumbo la Ukombozi,
mahali ambapo hekima ya Mungu imetundikwa juu yake. Wanaalikwa kumwangalia Kristo
aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la
dhambi na mauti na hivyo kuwajalia tena uwezo wa kufanyika watoto wateule wa Mungu. Askofu
mkuu Balvo katika mahubiri yake ameendelea kukazia kwamba, imani ni zawadi kutoka
kwa Mwenyezi Mungu na ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na Kanisa. Imani hii inaweza
kurutubishwa kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti, Maisha adili yanayoongozwa na
Amri za Mungu pamoja na Sala inayojidhihirisha katika matendo. Wakatekumeni na
Wakristo katika ujumla wao, waendelee kuimarika katika imani, wakati wa raha na karaha;
wakati wa afya na magonja, daima Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza. Jumuiya
ya Wakristo wanaoishi CUEA wameombwa kuwasaidia Wakatekumeni wapya katika hija ya
maisha yao, ili hatimaye, waweze kupata ukomavu. Naye Monsinyo Pius Rutechura,
Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki na Kati, CUEA, amemshukuru
Askofu mkuu Balvo kwa kuwapatia heshima ya kutembelea CUEA na kushiriki katika Ibada
ya Misa Takatifu kama kielelezo cha kufunga Mwaka wa Imani, tayari kuendeleza neema
na baraka ambazo waamini wamejipatia wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.