2013-11-24 15:14:19

Waamini wanaoteseka kutokana na imani kwa Kristo na Kanisa lake, wakumbukwa na Papa!


Mara baada ya Maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu sanjari na kufunga Mwaka wa Imani, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu aliwatakia kheri na baraka wote waliomiminika kwa wingi katika Ibada ya Misa Takatifu kutoka ndani na nje ya Italia.

Amewasalimia kwa namna ya pekee, washiriki wa kongamano la kitaifa la Huruma ya Mungu; Jumuiya ya waamini kutoka Ucrain, wanapofanya kumbu kumbu ya miaka 80 tangu ilipotokea njaa kubwa inayojulikana kama "Holodomor" iliyosababisha watu zaidi ya millioni moja kupoteza maisha.

Baba Mtakatifu amewakumbuka Wamissionari kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliojitosa kimasomaso kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia. Kati yao amemkumbuka Mwenyeheri Junìpero Serra, Mmissionari kutoka katika Shirika la Wafranciskani anayekumbukwa kwa kutimiza miaka mia tatu tangu alipozaliwa. Katika sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu amewakumbuka waamini wote wanaoteseka na kudhuliwa kutokana na imani na uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.