2013-11-24 09:07:01

Ugonjwa ni mahali pa kuonja fadhila za Kimungu: imani, matumaini na mapendo!


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski katika tafakari yake wakati wa Maadhimisho ya Mkutano wa XXVIII wa Kimataifa uliondaliwa na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya uliohitimishwa mwishoni mwa Juma, anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni chachu ya kuendeleza mambo msingi ambayo waamini wametafakari na kuonja katika hija ya maisha yao ya kiroho na kimwili kwa mwaka mzima, ili waweze kuyaendeleza kwa siku za usoni kadiri ya Mpango wa Mungu.

Anawahamasisha wagonjwa na wale waliokata tamaa ya maisha kutokana na shida na majaribu mbali mbali, kuutafuta tena mwanga wa imani unaojikita katika upendo na matumaini ya kweli kwa Mwenyezi Mungu, daima wakiwa tayari kupokea na magonjwa kama sehemu ya kushiriki katika kazi ya ukombozi, iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake! Imani anasema Baba Mtakatifu Francisko, iwe ni dira na mwanga wa maisha ya waamini kwa kutambua kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwathamini hata katika magonjwa na mahangaiko yao ya ndani!

Ugonjwa unaweza kuwa ni mahali muafaka pa kuonja na kufanya mang'amuzi ya kweli za kiimani pamoja na mahusiano ya kibinadamu ndani ya Jamii. Kuna umuhimu wa kuonesha ubinadamu unaojali na kuguswa na mahangaiko ya wengine na kwa namna ya pekee kabisa wagonjwa na wale wasiokuwa na msaada. jambo la kusikitisha ni kuona ukatili unaoendelea kufanywa dhidi ya wagonjwa kana kwamba, wao wamependa kuwa katika hali hii na wengi wanasahau kwamba, kabla hujafa, bado mwanadamu hujaumbika!

Askofu mkuu Zygmunt anaendelea kubainisha kwamba, ugonjwa ni mahali pa kuonja kwa namna ya pekee zile fadhila za Kimungu, yaani: imani, matumaini na mapendo. Katika mateso na mahangaiko ya ndani, mgonjwa anaweza kuwa ni kielelezo makini cha imani kwa Kristo na Kanisa lake, lakini pale anapokata tamaa matokeo yake ni kukimbilia kwa wachawi na imani za kishirikina.

Waamini watambue na kuonja nguvu na ukuu wa Mungu hata katika mateso na magonjwa yao, kwani Yeye ana uwezo wa kuwainua na kuwanyanyua tena. Magonjwa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, lakini yanaweza kupatiwa maana kadiri ya imani na matumaini aliyo nayo mgonjwa mwenyewe. Imani inamwangazia mgonjwa hata katika giza la undani wa maisha yake, kwa kutambua kwamba, daima Mwenyezi Mungu anafanya hija na watu wake, kamwe hawezi kuwatelekeza, jambo la msingi ni kufungua macho ya imani, ili kutambua uwepo wa Mungu anayeokoa na kuponya.

Wagonjwa wapate faraja kutoka katika familia na Jamii inayowazunguka anasema Askofu mkuu Zygmunt Zimowski katika tafakari yake kwa wajumbe waliokuwa wanahudhuria mkutano wa kimataifa wa XXVIII uliokuwa unajadili pamoja na mambo mengine mchango wa Kanisa katika kuwahudumia wazee wagonjwa!







All the contents on this site are copyrighted ©.