Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, waamini wamepata fursa ya kusikiliza shuhuda
na changamoto katika hija ya imani mintarafu historia ya Kanisa. Waamini wengi hasa
kutoka Makanisa ya Mashariki walishuhudia imani yao kwa Kristo kwa njia ya kumwaga
damu.
Hii ni kutokana ukweli kwamba, Mwanga ambao ni Kristo ulikuja kuleta
nuru ulimwenguni, lakini kwa bahati mbaya mwanadamu akapenda kugandamana na giza na
kuitema zawadi ya mwanga. Yesu ambaye ni Mkombozi na chemchemi ya matumaini ya ulimwengu
akawekwa pembeni utadhani ni gari bovu!
Ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na
Kardinali Leonardi Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya
Mashariki wakati alipokuwa anashiriki kwenye Kongamano lililoandaliwa na Kanisa Katoliki
la Kigiriki kutoka Romania kwa kuongozwa na kauli mbiu "Imani na Kifodini" wakati
wa utawala wa Kikomunisti nchini Romani. Mama Kanisa anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa
ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ambayo yametoa nafasi kwa waamini kufanya tafakari
ya kina, kutolea ushuhuda wa imani tendaji pamoja na kusonga mbele, huku wakitembea
katika mwanga wa Kristo Mfufuka.
Kardinali Sandri anasema, viongozi wa Kanisa
waliwaandaa watu kusimama kidete kulinda na kutetea imani yao hata ikiwabidi kutolea
sadaka ya maisha! Maandalizi haya yalijikita katika mahubiri kwenye Ibada za Misa
takatifu, hija za kichungaji zilizofanywa na Maaskofu Maparokiani, hija za maisha
ya kiroho pamoja na barua za kichungaji zilizowahamasisha waamini kutoa kipambele
cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake, matokeo ni watu wakaimarika katika imani kiasi
cha kujitosa kimasomaso kukabiliana na udhalimu wa nyakati zile.
Kilele cha
madhulumu haya ni mwaka 1948 Wakristo walipohukumiwa kwa "mpigo" kifo dini bila hata
ya kesi yao kusikilizwa. Waamini waliteseka na kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo,
Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kila Askofu akawa imara na wala hakukubali kumsaliti
Kristo na Kanisa lake, changamoto ya kuendelea kudumisha misingi thabiti ya imani,
kiasi hata cha kutolea ushuhuda katika imani tendaji bila kusahau kukuza majadiliano
ya kidini na kiekumene, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.