2013-11-24 08:27:01

Miaka 50 ya Waraka wa Amani Duniani: mambo msingi: ukweli, haki, upendo na uhuru!


Majadiliano na demokrasia ni nyenzo muhimu sana katika kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani Barani Ulaya, kwani, watu wengi wanashirikishwa katika mchakato wa kudumisha haki na nyajibu ndani ya Jamii kwa ajili ya mafao ya wengi. Kwa njia hii Mwenyezi Mungu anapata utukufu na amani inadumu miongoni mwa watu wake.

Ni maneno ya Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati alipokuwa anachangia mada kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII alipochapisha Waraka juu ya Amani Duniani, Pacem in Terris, Kongamano lililoandaliwa na Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno, hivi karibuni.

Ni Waraka uliotolewa wakati ambapo dunia ilikuwa inashuhudia kinzani na vitisho vya vita ya kinyuklia. Papa Yohane wa XXIII akapiga moyo konde, akwaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa nafasi kwa ajili ya majadiliano ili kujenga misingi ya haki, amani na utulivu, utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Katika waraka huu, Papa Yohane wa XXIII alikazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kujenga na kudumisha mahusiano dhabiti kati ya watu wa mataifa kwa kujikita katika ukweli, haki, upendo na uhuru wa kweli, kwani haya ni mambo msingi yanayogusa uwajibikaji wa kimaadili katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu.

Jamii inapaswa kujenga pia utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia ya kudumisha misingi ya haki na amani, kwani kwa miaka ya hivi karibuni, dini zimekuwa ni chanzo kingine cha kuvurugika kwa amani kati ya watu hasa kutokana na misimamo mikali.

Kardinali Peter Turkson anasema, Waraka wa Amani Duniani, unatoa changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika mikakati yao na kamwe wasimweke pembezoni, kwani wanaweza kujikuta wakitumbukia kwenye majanga na maafa makubwa. Waraka wa Amani Duniani ni kati ya nyaraka muhimu sana zilizotolewa na Mama Kanisa mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa na umuhimu wa wanasiasa kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya mafao ya wengi.

Mwenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II wanatarajiwa kutangazwa na Mama Kanisa kuwa Watakatifu hapo tarehe 27 Aprili 2014 mjini Vatican. Hawa ni kati ya viongozi wakuu wa Kanisa waliohamasisha misingi ya haki, amani na utulivu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, wakati ambapo mtutu wa bunduki ulikuwa unaendelea kutishia usalama wa maisha ya watu!







All the contents on this site are copyrighted ©.