Kampeni ya amani katika Eneo la Maziwa Makuu kuzinduliwa hapo tarehe Mosi, Desemba
2013
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, ACEAC, linalounganisha
nchi za: DRC, Burundi na Rwanda, linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kushuhudia imani yao kwa Yesu Kristo na Kanisa lake; kuanzisha mchakato wa ujenzi
wa mshikamano na mfungamano wa kijamii pamoja na kusaidia majiundo makini ya dhamiri
nyofu, ili watu waweze kusamehe na kusahau sanjari na kujenga utamaduni na misingi
ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa!
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
katoliki Afrika ya Kati, hapo tarehe Mosi Desemba 2013, Jumapili ya kwanza ya Kipindi
cha Majilio, litazindua mpango mkakati unaopania kujenga na kudumisha misingi ya amani
kwenye Eneo la Maziwa Makuu, tukio hili litafanyika mjini Goma, Kaskazini mwa Kivu.
Takwimu zinaonesha kwamba, nchini DRC kuna jumla ya watu millioni 5 waliofariki dunia
katika kipindi cha miaka kumi na mitano iliyopita na watu zaidi ya millioni mbili
na nusu hawana makazi ya kudumu. Idadi ya nyanyaso na madhulumu dhidi ya wanawake
katika eneo hili inazidi kuongezeka kutokana na vita pamoja na machafuko ya kisiasa
na kijamii.
Vyama vya kiraia hivi karibuni, viliiomba Serikali ya DRC Jumuiya
ya Kimataifa na Majeshi ya waasi kuhakikisha kwamba, wanapata suluhu ya kudumu, ili
amani iweze kutawala tena nchini DRC kwani kinzani, migogoro na vita ni "janja" ya
watu wacheche wanaoendelea kufaidi wakati mamillioni ya watu yanateseka kutokana na
vita. Mkakati wa amani kwenye Eneo la Maziwa Makuu unaungwa mkono pia na viongozi
wa Kanisa Anglikani na uko wazi kwa watu wenye mapenzi mema kuchangia ili amani ya
kweli iweze kupatikana.
Ufafanuzi huu umetolewa na Askofu Fridolin Ambongo
Besungu wa Jimbo la Bokungu - Ikela, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya kati na Mratibu wa Kampeni "Amani katika
Eneo la Maziwa Makuu". Viongozi wa kidini nchini DRC wanawapongeza wadau mbali mbali
kutokana na mafanikio yaliyopatikana hivi karibuni baada ya ngome ya M23 kuchakazwa
vibaya.
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuunga mkono juhudi za kutafuta amani
ya kudumu nchini DRC sanjari na kuanza mchakato wa: haki, amani, upendo na upatanisho
wa kweli. Watu wajifunze kuheshimu haki msingi za binadamu sanjari na kujenga utamaduni
wa amani na utekelezaji wa dhamana kwa kila mtu ndani ya Jamii.
Viongozi wa
kidini wanataka kurusha karata yao katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi
ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa nchini DRC, kwa kuwahusisha waamini wa Makanisa
yao, viongozi wa kisiasa na kiserikali pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Jitihada
hizi ni ushirikiano na Mashirika ya misaada ya kiutu CAFOD kutoka Uingereza na CatholicRelief
Service, CRC kutoka Marekani.