2013-11-23 08:52:23

Nendeni mkafundishe na kuwaponya wagonjwa!


Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahudumu wa sekta ya afya katika Maadhimisho ya Mkutano wa XXVIII wa Kimataifa, uliokuwa unafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 23 Novemba 2013, limezindua kitabu cha msaada kwa ajili ya wahudumu wa sekta ya afya na Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza imani.

Msaada huu wa kichungaji unaongozwa na kauli mbiu "Nendeni, mkafundishe na kuwaponya wagonjwa, Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo. 10: 6-8. Kauli mbiu hii kwa lugha ya Kilatini inasomeka kama ifuatavyo: "Euntes docete et curate infirmos". Huu ndio msingi wa utume wa Mama Kanisa katika kuwahudumia wagonjwa kama alivyofundisha Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake.

Wagonjwa wanapaswa kushibishwa kwa utamu wa Neno la Mungu na tiba muafaka ndivyo anavyofafanua Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahudumu wa sekta ya afya wakati wa kuzindua kitabu hiki kinachopania kuwa ni msaada wa kichungaji kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, wakati huu Mama Kanisa anapojielekeza zaidi katika azma ya Uinjilishaji Mpya.

Huduma ya Neno la Mungu na tiba ni mambo yanayokwenda pamoja, lakini kwa namna ya pekee wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na mwendelezo wa mchakato wa Uinjilishaji Mpya, changamoto kubwa kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Vituo vya huduma ya afya vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa ni mahali muafaka pa Uinjilishaji; mahali ambapo watu wanaweza kuonja upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya jirani zao. Wahudumu wa sekta ya afya watambue kwamba, wao ni watume wa huruma ya Mungu kati ya watu wanaoteseka na kusumbuka!

Monsinyo Jean Marie Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahudumu wa sekta ya afya anasema, mikakati ya kichungaji katika sekta ya afya na Uinjilishaji kama sehemu ya mchakato wa kutangaza imani ni mambo muhimu sana kwa Mama Kanisa kwa wakati huu. Hiki ni kitabu chenye kurasa 48 ambazo zimesheheni tafakari za kina mintarafu Mwaka wa Imani na Uinjilishaji Mpya.

Huu ni msaada wa pekee kabisa kwa wahudumu wa sekta ya afya, watu wa kujitolea pamoja na familia zenye wagonjwa, zinazo tamani kufanya maboresho ya huduma ya kiroho wanayotoa kwa ajili ya wagonjwa wanaowahudumia. Kitabu hiki kimezinduliwa wakati wa mkutano wa Kimataifa wa XXVIII uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu "Kanisa kwa ajili ya huduma kwa wazee wagonjwa: tiba kwa wagonjwa walioathirika na magonjwa ya mishipa ya fahamu. Kitabu hiki ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ambao unafungwa rasmi kwa Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu.

Kitabu kinajikita zaidi katika mikakati ya shughuli za kichungaji kama sehemu muafaka ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, anasema Monsinyo Mupendawatu. Mama Kanisa anapenda kushika hatamu katika kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa kwenye ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; ili kuyatakatifuza malimwengu!

Umefika wakati wa kuanza tena maisha mapya kwa Yesu Kristo kwa njia ya kusoma, kuitafakari na kuimwilisha Injili ya Huruma ya Mungu katika kila hatua ya historia ya maisha ya mwanadamu na kwamba, matunda yake ni: toba na wongofu wa ndani, faraja na matumaini yasiyodanganya kamwe!







All the contents on this site are copyrighted ©.