2013-11-23 14:06:22

Michezo ni furaha, kamwe isipimwe kwa vigezo vya kiuchumi, itakosa dira na mwelekeo sahihi!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 23 Novemba 2013 amewashukuru wajumbe wa Kamati ya Michezo ya Olimpic kutoka Ulaya kwa jitihada zote wanazofanya kwa njia ya michezo kwa ajili ya kumwendeleza mwanadamu pamoja na kudumisha udugu na kwamba, kuna uhusiano wa dhati kati ya Kanisa na michezo.

Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa michezo katika makuzi ya mwanadamu mzima: kiroho na kimwili; inamwondolea mtu dhana ya ubinafsi na hivyo kumjengea moyo wa sadaka na majitoleo, huku akijitahidi kujenga uhusiano na urafiki pamoja na jirani zake; kwa kuheshimu sheria. Hii ni changamoto kwa wadau wa michezo katika ngazi mbali mbali kuhakikisha kamba, wanajitahidi kujenga na kukuza tunu msingi za kiutu na kidini msingi wa Jamii yenye haki na mshikamano wa dhati.

Hii inatokana na ukweli kwamba, michezo ni lugha ya kiulimwengu, inayovuka mipaka ya lugha, kabila, dini na siasa; ina uwezo wa kuwaunganisha watu na hivyo kujenga majadiliano na ukarimu. Hii ni tunu muhimu sana katika maisha ya Kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wadau mbali mbali wa michezo kuhakikisha kamba, wanawajengea vijana wa kizazi kipya utamaduni wa amani, ushirikiano na hali ya kuishi kwa utulivu, kwani lengo la michezo ni kujenga na wala si kubomoa kama inavyojionesha kwenye bendera ya michezo ya Olimpic. Michezo isipimwe kwa vigezo vya uchumi na kutafuta ushindi kwa gharama zote, kwani matokeo yake ni kukosa dira na mwelekeo sahihi. Wanamichezo wanakosa maana halisi na furaha ya michezo. Michezo ni furaha anasema Baba Mtakatifu na wala si kisima cha utajiri.

Wadau wa michezo wanapaswa kujenga utamaduni unaoheshimu na kuthamini moyo wa shukrani, sheria maadili na uwajibikaji. Baba Mtakatifu amewatakia kheri na baraka wanamichezo wote watakaoshiriki kwenye michezo ya Olimpic kutoka sehemu mbali mbali za dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.