Imani na amani ni chanda na pete, kamwe haviwezi kutenganishwa!
Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano maalum
na Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa anapofunga Mwaka wa Imani anabainisha kwamba,
Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu ni changamoto kwa waamini kutafakari tena
fadhila za Kimungu na Kibinadamu na kuona kama kweli wanashiriki kikamilifu katika
ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwani hakuna haki pasi na amani na hakuna amani pasi na
haki.
Fadhila ni
msimamo wa kudumu tena imara unaomchangamotisha mwamini kutenda mema. Fadhila za kibinadamu
ni hali thabiti, na maelekeo imara ya akili na ya utashi zinazotawala matendo ya binadamu,
zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo wa mwamini wa kufuata akili na imani. Fadhila
hizi zinafumbatwa katika maisha adili, zinatakaswa na kuinuliwa na neema ya Mwenyezi
Mungu.
Haki ni kati ya fadhila za binadamu; ni nia na utashi wa kudumu na imara
wa kuwapa wengine wanachostahili. Haki kwa Mwenyezi Mungu inaitwa "fadhila ya dini".
Yesu ni Mfalme wa Haki na Amani changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anajenga
na kudumisha utamaduni wa kutenda haki. Kila mtu anahamasishwa kuwa ni mdau wa Haki
Jamii, ukweli na uwazi! Mama Kanisa anapohitimisha Mwaka wa Imani, anawaalika waamini
kuendelea kuombea misingi ya haki na amani anasema Askofu mkuu Lebulu.
Imani
ni fadhila ya Kimungu ambayo kwayo mwamini anamsadiki Mwenyezi Mungu na kila kitu
ambacho amekifunua na Kanisa linawataka waamini kusadiki, kwani Mungu ndiye utimilifu
wa ukweli wenyewe. Mwanadamu anapaswa kufahamu na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika
maisha yake, kwani imani hutenda kazi kwa upendo. Ufalme wa Kristo unafumbatwa katika
imani na utakatifu wa maisha.
Askofu mkuu Josephat Lebulu katika tafakari
kuhusu Sherehe za Kristo Mfalme anahitimisha kwa kusema kwamba, amani na imani ni
chanda na pete, ndiyo maana kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru
wa kuabudu, kwani huu ni msingi wa haki nyingine zote za binadamu.