2013-11-22 08:28:58

Yesu Kristo ni Mfalme wa ukweli na uzima; utakatifu na neema; haki, mapendo na amani!


Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano na Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kufunga Mwaka wa Imani sanjari na Siku kuu ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu, anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu sifa na ukuu unaosimuliwa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Kristo Mfalme, hili ujumbe huu uweze kuwa kweli ni dira na mwongozo katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Yesu Kristo ni Mfalme wa ukweli, waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni wajumbe wa ukweli. Yesu ni Mfalme wa uzima anayewakirimia waja wake maisha tele! Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kukumbatia na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba, nyanyaso, madhulumu pamoja na kutothamini utu na heshima ya binadamu.

Yesu Kristo ni Mfalme wa Neema na kwamba, yuko tayari kuwakirimia waja wake neema na baraka wanazohitaji katika hija ya maisha yao hapa dunia, ikiwa kama watakuwa na moyo radhi, tayari kumsikiliza kutoka katika undani wa maisha yao. Kwa sifa hizi, Askofu mkuu Lebulu anawataka waamini wakati huu Mama Kanisa anapoufunga Mwaka wa Imani, kuzipatia sifa hizi umuhimu wa pekee katika vipaumbele vya maisha yao kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha matakatifu na adili.







All the contents on this site are copyrighted ©.