2013-11-22 07:58:13

Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu


Ninakuleteeni habari njema ya furaha tunapotafakari pamoja ujumbe wa Neno aliyefanyika mwili, Mfalme wa mbingu na nchi. Ni Dominika ya 34 ya mwaka C iliyo pia sherehe ya Yesu Kristu Mfalme. RealAudioMP3
Kanisa linashangilia na kusherehekea utukufu wa Mwana wa Mungu, Yesu Kristo Mfalme. Kanisa linatangaza daima utawala na enzi ni vya Yesu Kristu Mfalme na hivi lajiweka chini ya uongozi wake aliye kichwa na mwanga katika safari ya kuelekea mbinguni. Pamoja na tangazo hilo Kanisa latuhimiza kumfuata Yesu Kristu Mfalme, kukiri ukuu wake wazi wazi machoni pa mataifa lililo hasa lengo la sherehe hii.
Mpendwa msikilizaji, ufalme wa Kristo kadiri ya prefasio tunayoitumia katika sherehe hii ni ufalme wa ukweli, maisha, utakatifu, neema, haki, upendo na amani. Basi mwaliko kwetu ni kuyaishi haya na hasa kuyatangaza kwa njia ya ushuhuda na si maneno matupu. Oneni jinsi Bwana anavyoishi hayo mpaka pale msalabani.
Mama Kanisa ameweka sherehe hii mwishoni mwa kipindi cha mwaka ili yote yakamilike katika yeye. Tukirudi kidogo katika historia tunaona kuwa sherehe hii iliwekwa katika Kanisa na Baba Mtakatifu Pio XI mnamo mwaka 1925, Kanisa likitaka kujibu tawala za kisiasa, kipagani na kidikiteta ambazo zilikuwa zikikataa utawala wa Mungu na utawala wa Kanisa.
Mpendwa msikilizaji pamoja na kuzaliwa kwa sherehe hii ya Yesu Kristu Mfalme katika mazingira kama hayo, bado kilichomo ndani ya sherehe hiyo ni cha zamani yaani, tangu mwanzo wa ukristu. Wakristu wa kwanza walikuwa katika maisha yao wakitamka kuwa “Yesu ni Bwana” na kwa namna hiyo wengi wakafa mashahidi katika harakati za kutaka kumtukuza Bwana Mfalme wa mbingu na nchi.
Mpendwa msikilizaji Yesu Kristo Mfalme ndiye yule mchungaji mwema ambaye daima tunakutana naye katika sura 10 ya Injili ya Mt. Yohane ambaye ajua sauti ya kondoo wae na walio wake waijua sauti yake. Kumbe ni mfalme wa amani na mapendo.
Nabii Ezekieli anatupa picha halisi ya mfalme aliye pia mchungaji mwema, aliye kinyume na wafalme wa dunia. Mchungaji wa kondoo anayetabiriwa na Ezekieli ni yule ambaye anatafuta kundi lake lililopotea na kulirudisha katika malisho safi na baadaye kulisalimisha pia nyumbani. Kundi hili la kondoo ni wagonjwa, waliopotea waliovunjika moyo na waliofukuzwa.
Picha hii ya mchungaji inajitokeza katika Yesu Kristu Mfalme ambaye kwa Njia ya Msalaba watu wote wamerudishwa nyumbani. Kumbuka maneno yake alipokuwa akizungumza na Nikodemo “kama vile Musa alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani naye mwana wa mtu atainuliwa juu vivyohivyo ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele” Yn 3:14-15
Katika somo la pili Mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho anatualika kusadiki kuwa Kristu ndiye limbuko letu. Ndiye ambaye amebatilisha kifo kwa njia ya msalaba wa ushindi kama ambavyo walatini wanasema “regnaviti a ligno Deus”. Anaonesha ufalme na ukuu wake kwa kushinda kifo kilicholetwa duniani kwa njia ya Adamu. Kwa ushindi dhidi ya kifo Mungu amemtukuza na kumwadhimisha mno, na hivi mwishoni mwa dunia utawala wa shetani utashindwa kabisa.
Mtume Paulo hatangazi jambo jingine bali kuwa Yesu Kristu ni Mfalme ambaye Kanisa lamshangilia na kumtukuza kwa shangwe na vigelegele. Sisi wanakanisa tunapaswa kufuata mtililiko huohuo pasipo mashaka tukitangaza ushindi wa Bwana, ambaye ametutoa katika ufalme wa giza na kutupeleka katika ufalme wa mwanae ambao kwao tumepata ukombozi na ondoleo la dhambi.
Mwinjili Mathayo anatuonesha mfalme mwenye mamlaka juu ya mbingu na dunia, mwenye uwezo wa kutoa hukumu kadiri ya upendo na haki. Mfalme huyu ameketi katika kiti cha enzi akiwabagua mataifa yote, wengine mkono wa kulia na wengine mkono wa kushoto. Ndiyo kusema kwanza ana enzi na mamlaka lakini pia ni mwenye haki.
Katika hukumu anayotoa yapo mambo msingi ambayo anayatazama. Kama mmoja aliwalisha maskini au hapana, kama mmoja aliwatazama wagonjwa ambao ni kielelezo cha uwapo wa sauti ya Mungu katikati ya jumuiya ya watu. Kigezo kingine ni kile cha kuwatazama wafungwa kifungoni, walio utumwani na wenye njaa. Kwa wale ambao waliwahudumia wahitaji hawa, atawaambia kaeni mkono wa kulia na mkapate kula vilivyo vya Baba yangu maana nilipokuwa mgonjwa mlikuja kuniona hospitali. (Kumbuka kuwa mtu ni sura na mfano wa Mungu).
Kwa hakika ukitazama vema lengo la ainisho hili la watu mbalimbali waliowahitaji, utagundua nguzo kuu, ambayo humwezesha mmoja kuingia katika ufalme wa Mbinguni, nayo ni MAPENDO KWA JIRANI NA KWA MUNGU. Ni kushuhudia kwa dhati IMANI katoliki, imani tendaji, imani inayokuza ubatizo hadi mwisho wa nyakati. Ni kubaki katika pendo la Mwana wa Mungu katika kuhudumu waliowake.
Mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, kabla ya kumalizia tafakari yetu yafaa pia kutambua hakikisho la kuwa yeye ni Mfalme kadi ya Injili . Mwinjili Matayo anasema akinukuu maneno ya watesi wa Bwana “Huyu ni mfalme wa Wayahudi” na baadaye yanafuata maneno “Kama wewe ni mfalme wa Wayahudi jiokoe mwenyewe”. Bila kutambua, watesi hawa wakidhani wanammalizia na kumpatiliza Mwana wa Mungu, wanatuhakikishia kuwa yeye ni Mfalme wa Mbingu na nchi na ni mfalme wa Wayahudi. Walitarajia afanye miujiza kuhakikisha ufalme wake na badala yake anachagua msalaba wa wokovu kwa watu.
Mpendwa, katika hilo kumbukeni yule mwizi pale msalabani anayesema “Yesu nikumbuke katika ufalme wako….” Na Bwana wetu Yesu Kristu Mfalme anahitimisha katika kumwokoa mtu akisema tutakuwa pamoja mbinguni. Mpendwa unayenisikiliza je, huyu Mfalme Yesu Kristu anatawala moyoni mwako, je sauti yake “tutakuwa pamoja mbinguni unaisikia?” Je, ndugu yangu mpendwa, unaishi kwa ajili ya Bwana au unaishi kwa ajili yako mwenyewe? Kuishi kwa ajili yako mwenyewe maana yake unacho chanzo chako mwenyewe na mwisho wako mwenyewe! Hicho kwa hakika ni kifo!
Mpendwa msikilizaji, leo hii Mama Kanisa anafunga mwaka wa Imani, mwaka ambao Mama Kanisa kwa njia ya Papa Benedikto wa XVI uliwekwa rasmi ili kwao tuchote fadhila ya imani, tukakuze fadhila hiyo na kisha kuieneza kwa mataifa. Imani ni kusadiki kabisa tukiwa na hakika ya mamb tunayoyatumainia, ni kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona. Na kwa namna hayo tunaweza kupata kibali cha Mungu kama wazee wetu wa zamani walivyopata kibali cha Mungu kwa njia ya imani. Papa Francesco anasema imani mwanga ambao upo tangu kuumbwa kwetu na mwanga huo huendelea kukua mpaka mwisho wa nyakati, ni Kristu mwanga wa mataifa.
Katika Barua yake hiyohiyo ya kitume LUMENI FIDEI Papa
Francisko kisha anasema, imani si tu huangazia a mambo ya ndani ya Kanisa, au kutumika tu katika kujenga mji wa milele, lakini pia husaidia kujenga jamii yetu katika njia ya uhakika kwa jamii, kutembea vyema kuelekea mustakabali wa maisha yenye matumaini.
Anaendelea kuangalisha katika manufaa ya familia na jamii , kwamba, kuirejesha imani katika familia, inakuwa ni uwasilishaji wa uwezo wa mwanga, wenye kumulikia mahusiano katika jamii nzima. Ni kuiwezesha familia na jamii kufanya majiundo adilifu na manufaa ya wote. Huanzia katika jamii kutembea katika njia ya udugu, kwenye muono kwamba, sisi sote ni wana wa Baba Mmoja wa mbinguni.

Mpendwa msikilizaji, tunaposherehekea Sherehe ya Mfalme wetu na kufunga mwaka wa imani tukumbuke kuwa yeye anapaswa kutawala katika familia zetu zote, katika maneno yetu na matendo yetu. Maneno kama “ mteja ni mfalme” yafaa kuangaliwa vizuri kama kweli yanakuza ufalme wa Kristu au ufalme wetu sisi wenyewe! Yafaa kuangalia ni huduma gani tumefanya katika Kanisa kwa kipindi cha mwaka wa Imani. Ndiyo kusema hatujachelewa bado twaweza kuanza upya safari ya imani. Kumbukeni Bwana anayemwokoa mtu kwa njia ya msalaba anakutaka na wewe uwe chombo cha amani na upatanisho kama tunda la imani.
Tunawatakieni heri na baraka Waamini wote na zaidi wale ambao parokia zao na makanisa yao yako chini ya somo Yesu Kristo mfalme. Mkashike imani na mkawe mfano wa kuigwa mkiongozwa na Yesu Kristo mfalme wa Amani. Tumsifu Yesu Kristo Mfalme.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.