Mafundisho Jamii ya Kanisa ni nguzo ya haki jamii inayodumisha: utu na heshima ya
binadamu
Mafundisho Jamii ya Kanisa ni utajiri mkubwa unaofundishwa na Mama Kanisa katika masuala
yanayogusa usawa na utofauti katika maisha ya mwanadamu kama njia ya kuonesha mshikamano
wa dhati katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Watu
wanapaswa kutambua na kuthamini tofauti zinazojitokeza katika maisha yao sanjari na
kutambua umuhimu wake katika utandawazi na kwamba, kila mtu anayo nafasi ya pekee
katika Jamii inayomzunguka. Vijana wanaonesha jeuri na nguvu ya kusonga mbele kwa
matumaini na ari kuu zaidi, wakati ambapo wazee ni hazina ya hekima na busara; kumbe,
wanapaswa kutegemezana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jamii husika.
Vijana
wasiokuwa na ajira ambao ni asilimia kubwa katika jamii ni janga la kimataifa kwa
siku za usoni. Ni watu wasiokuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, jambo
linalohatarisha amani na usalama kwa Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni sehemu ya ujumbe
uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Tamasha la tatu la Imani,
lililofanyika mjini Verona, Alhamisi, tarehe 21 Novemba 2013.
Baba Mtakatifu
anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa ni rejea katika medani mbali mbali za maisha kama
sehemu ya mchakato wa waamini walei kuyatakatifuza malimwengu badala ya kuwa na uchu
wa mali na madaraka pamoja na baadhi ya watu kutafuta faida kubwa. Mafundisho Jamii
ya Kanisa yanayosheheni tafakari za Imani yanapania kuwajengea waamini na watu wenye
mapenzi mema uhuru wa ndani na dhamiri nyofu, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza
kwa utu na heshima ya binadamu; wakijitahidi kuongozwa na kanuni auni, ili kujenga
na kudumisha matumaini kwa wale waliokata tamaa.
Baba Mtakatifu anasema Mafundisho
Jamii ya Kanisa yanapania kujenga na kudumisha haki jamii, maendeleo endelevu ya watu
pamoja na kushiriki katika mchakato wa kutengeneza fursa za ajira kwa kuondoa mambo
yote yanayokwamisha utekelezaji wa haki jamii.
Ni mafundisho yanayokazia mshikamano
wa kidugu baina ya watu wa mataifa. Mshikamano kwa wachumi ni jambo linaloonekana
kuwa kama fedheha. Watu wajenge na kuimarisha mshikamano na ushirikiano kama njia
ya kupambana na changamoto mbali mbali za maisha mintarafu usawa na utofauti. Waamini
na watu wenye mapenzi mema, hawana budi kujielekeza katika kukuza na kudumisha moyo
wa mshikamano na ushirikiano katika kukabiliana na majanga ya maisha; kwa kushuhudia
imani katika matendo.