Baba Mtakatifu Francisko anawaambia watumiaji wa mitandao ya kijamii kwamba, Ufalme
wa mbinguni ni kwa ajili ya watu wanaojiaminisha kwenye upendo wa Mungu na wala si
katika mambo ya kidunia.
Katika kilele cha Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu anatarajiwa,
Jumamosi jioni kuongoza Ibada ya kuwapokea Wakatekumeni kama kielelezo cha kuvuka
Mlango wa Imani, tayari kumpokea Kristo katika hija ya maisha yao ya Kikristo. Ibada
hii inatarajiwa kuhudhuriwa na wakatekumeni kutoka sehemu mbali mbali za dunia kama
kielelezo cha Ukatoliki wa Kanisa la Kiulimwengu.
Jumapili asubuhi, kwa mara
ya kwanza waamini watapata fursa ya kutolea heshima kwa masalia yanayosadikiwa kuwa
ni ya Mtakatifu Petro, Mwamba wa Imani, aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo
na Kanisa lake. Ilikuwa ni Mwaka 1971, Papa Paulo VI alipopewa masalia haya yanayohifadhiwa
kwenye Kikanisa cha Papa na kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Siku kuu ya Watakatifu
Petro na Paulo miamba wa imani masalia haya hupelekwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican.
Katika Sherehe ya Kristo Mfalme wa Dunia, Baba Mtakatifu
Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha kufunga Mwaka
wa Imani, Ibada inayotarajiwa kuanza saa 4:30 kwa saa za Ulaya. Katika Ibada hii,
Baba Mtakatifu atawagawia baadhi ya waamini Waraka wake wa kichungaji baada ya Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani unaojulikana kama "Furaha ya Injili" "Evangelii Gaudium", itakayozinduliwa
rasmi, Jumatatu ijayo hapa mjini Vatican.