Jitahidini kumwabudu Mungu kwa ibada, usikivu, tafakari, toba na wongofu wa ndani,
ili kupokea msamaha na upendo wa Mungu!
Hekalu ni mahali patakatifu panapotumiwa na waamini kwa ajili ya kumwabudu, kumshukuru
na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Mwili wa binadamu ni hekalu la Fumbo la Utatu Mtakatifu,
mwaliko kwa waamini kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayezungumza kutoka katika undani
wa maisha yao; tayari kufanya toba na kuomba msamaha ili kuendelea kumfuasa Mwenyezi
Mungu kwa njia ya Kristo.
Hekalu ni mahali pa rejea kwa waamini na Jamii husika
kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale. Jambo muhimu linalotekelezwa ndani ya Hekalu
au Kanisa si nyimbo au ibada inayofanyika humo, bali ni mkusanyiko wa Familia ya
Mungu inayoungana kuadhimisha Sadaka ya Misa Takatifu pamoja na kumwabudu Mwenyezi
Mungu, ambaye ndiye kiini rejea cha uwepo wa Kanisa au Hekalu.
Waamini wajibidishe
kumwabudu Mungu kutoka katika undani wa maisha yao kwa kuthamini utakatifu wa maisha
ya imani. Kamwe waamini wasimhuzunishe Roho Mtakatifu waliyempokea kwa Sakramenti
ya Ubatizo na Kipaimara. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu
Francisko Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko
mjini Vatican.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kujitakatifuza kwa
kutambua kwamba, kama binadamu wanaandamwa na dhambi. Mwamini anaweza kuboresha na
kuyatakatifuza maisha yake kwa njia ya sala, toba na wongofu wa ndani, ili kuonja
huruma na upendo wa Mungu unaotolewa kwa njia ya sakramenti ya Upatanisho na kuimarishwa
na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.
Kwa njia hii, waamini wanaweza kumwabudu
Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao: kwa ibada, usikivu na tafakari
ya Neno la Mungu; kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kuomba na kupokea msamaha, ambao
ni wimbo wa sifa kwa Mwenyezi Mungu.