Jengeni moyo, ari, bidii na udumifu katika sala, ili kuweza kushuhudia imani katika
matendo adili!
Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa, Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania katika mahojiano na Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa anapofunga
Mwaka wa Imani, anawaalika waamini kujenga na kudumisha moyo wa sala katika maisha
yao na kwamba, sala ni kwa ajili ya Familia nzima ya Mungu na wala hakuna upendeleo!
Anasema, Sala
inamwezesha mwamini kuinua moyo wake kwa Mwenyezi Mungu, kwa kumwomba mema yanaylingana
na matakwa yake. Hii daima ni zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayekuja kukutana
na mja wake katika undani wake wa maisha. Sala ya Kikristo ni fungamanisho hai na
Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Askofu msaidizi Nzigilwa anakiri kwamba, ingawa sala
ni muhimu sana katika maisha ya mwamini, lakini waamini wengi bado hawajajenga ari,
moyo, bidii na udumifu katika maisha ya sala na matokeo yake wanajikuta wakiogelea
katika visingizio vinavyowakwamisha kupata nafasi na muda wa kusali kwa dhati. Kusali
kunamwezesha mwamini kufunguliwa mifereji ya neema na baraka katika maisha yake.
Kumbe,
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani iwe ni kursa ya kukuza na kuimarisha ari na moyo wa
kupenda kusali zaidi, ili kupata nguvu ya kumshuhudia Mungu katika Imani, Liturujia
na Sakramenti za Kanisa, katika maisha adili na matakatifu na hatimaye, kuifanya sala
kuwa ni kielelezo cha imani tendaji.