2013-11-21 08:07:27

Tunu msingi za maisha ya kifamilia, kiutu na kimaadili zipewe msukumo wa pekee kwa Familia ya Mungu Barani Afrika!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya kati, ACERAC, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka, uliokuwa unafanyika mjini Libreville, Gabon, kwa kuendelea kuhimiza umuhimu wa Kanisa Barani Afrika kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia kama njia ya kutekeleza mapenzi ya Mungu kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.

Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, kuna ongezeko kubwa la talaka, kinzani na migogoro ya kifamilia katika majimbo yao, jambo ambalo linahitaji kuwa na mikakati makini ya shughuli za kichungaji kwa wanandoa watarajiwa sanjari na kuendeleza majiundo ya kiutu, kiroho na kimaadili kwa wajili ya familia za Kikristo ili ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Maaskofu wanasema kwamba, athari za utandawazi zinaanza kuzinyemelea Familia nyingi kiasi hata cha kusikia baadhi ya watu wakidai ndoa za jinsia moja, dhana ambayo ni ngeni sana katika mila na tamaduni nyingi za Kiafrika.

Watu wanaanza kukumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba; kuna ongezeko la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana, jambo linaloendekezwa na baadhi ya watu kutaka utajiri wa haraka haraka kwa gharama ya maisha ya watu wanyonge. Kutokana na kukua na kupanuka kwa miji mingi pamoja na pilika pilika za maisha ya mijini, wazazi wengi wamejikuta kwamba, hawana tena nafasi kubwa kwa ajili ya malezi na makuzi kwa watoto wao ndani ya Familia.

Maaskofu pamoja na mambo mengine wanaendelea kukazia majiundo makini kwa wanandoa watarajiwa, umuhimu wa tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti ndani ya Familia na kwamba, familia ni mahali muafaka pa ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano; ni mahali kukuza na kuimarisha sanaa ya kusikilizana, kusaidiana na kutaabikiana kwa hali na mali; kwa kuwajali wagonjwa na wazee; wajane na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Maaskofu wamesikitishwa sana na kasi kubwa ya kumong'onyoka kwa misingi bora ya maisha ya kifamilia, maadili na utu wema, kwa baadhi ya watu kutaka kukumbatia tamaduni za kigeni hata zile ambazo hazina tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Barani Afrika. Kutokana na changamoto zote hizi, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya kati limeamua kuanzisha Idara ya Familia itakayoshughulikia masuala ya kifamilia.







All the contents on this site are copyrighted ©.