2013-11-21 15:06:20

"Sitaweza kutulia hadi pale watu watakapoheshimiwa na kuthaminiwa; watakapopata mahitaji yao msingi, bila kupokonywa matumaini wala kulazimishwa kuzikimbia nchi zao"!


Kristo ni mwanga wa mataifa unaoshuhudiwa na Makanisa yote kutoka Mashariki hadi Magharibi na unaonekana katika kila nchi na taifa kwa njia ya waamini waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia, lakini wanaunganishwa pamoja kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Liturujia ya Makanisa ya Mashariki ina utajiri mkubwa wa: kitaalimungu, kitasaufi na sheria ambao inabubujika kutoka katika Mapokeo ya kitume hazina iliyorithishwa na Mababa wa Kanisa kwa ajili ya Kanisa.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na wajumbe wanaoshiriki mkutano wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Anawashukuru kwa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa. Katika mkutano huu, wajumbe wamepembua kwa dhati mchango wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na mchango wa Makanisa ya Mashariki, katika mchakato wa kutafuta umoja kamili miongoni mwa wafuasi wa Kristo, wakiongozwa na Roho Mtakatifu, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo, Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, hata pale inapowabidi kutoa sadaka kubwa.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa Makanisa Mahalia, lakini kipaumbele cha kwanza ni Ukulu wa kiti cha Mtakatifu Petro kinachosimamia ushirika wa mapendo, kwa kulinda tofauti za haki zilizopo, lakini zaidi kwa ajili ya huduma na kamwe tofauti hizi haziwezi kuathiri umoja wa Kanisa, bali zinaudumisha na kwamba, tofauti hizi ni muhimu katika ujenzi wa umoja wa Kanisa kama walivyokazia Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, amepata bahati ya kusikiliza ushuhuda wa viongozi wakuu kutoka katika Makanisa ya Mashariki kuhusu: madhulumu, ari na moyo wa kimissionari unaoendelea kuchipuka kutoka kwa waamini wa Makanisa ambayo kwa miaka mingi yamekuwa chini ya utawala gandamizi. Viongozi wanatakiwa kuandaa mikakati ya huduma za kichungaji kwa ajili ya waamini wanaoishi ughaibuni, ili kujenga na kuimarisha udugu na umoja miongoni mwa Wakristo wa Madhehebu ya Kilatini.

Baba Mtakatifu ameyapeleka mawazo yake Nchi Takatifu, mahali ambapo Yesu alizaliwa, akateswa na kufa Msalabani na kuwataka wakristo huko Mashariki ya Kati wasiuzimishe moto wa imani kutokana na kinzani na madhulumu wanayokumbana nayo katika hija ya maisha yao, bali wajenge na kuimarisha utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Kinzani, vita na migogoro ya kijamii na kisiasa Mashariki ya Kati ni kati ya mambo yanayomsikitisha sana Baba Mtakatifu.

Anasema, hataweza kutulia na kupata amani ya ndani hadi pale watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia watakapoheshimiwa na kuthaminiwa; watakapopata mahitaji yao msingi, bila kupokonywa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, wala kulazimishwa kuzikimbia nchi zao. Haki na uhuru wa kidini unapaswa kuheshimiwa kwani hata Wakristo wana haki ya kuendelea kuishi Mashariki ya Kati, ambako wameendelea kukiri imani yao kwa Yesu Kristo kwa takribani miaka elfu mbili iliyopita. Ni watu wanaopaswa kushirikishwa katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu amewataka viongozi wa Makanisa ya Mashariki kuendelea kuwa macho na kwamba, iko siku Mwenyezi Mungu atawakirimia msaada wake unaobubujika kutoka kwa Mungu ambaye ni mwingi wa huruma, upatanisho na amani. Sala ina nguvu inayoanzisha majadiliano pale ambapo kuna kinzani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kilio cha sala yao kitaweza kusikiwa na Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa.

Mwishoni baba Mtakatifu Francisko, amewaweka wananchi wa Mashariki ya Kati chini ya maombezi ya wenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II, ili aweze kuwaombea kwa njia ya Bikira Maria aliyewakirimia Mfalme wa Amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.