Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Novemba, inaadhimisha Siku ya Wavuvi
Duniani. Lengo ni kuwaenzi wavuvi wanaotekeleza wajibu wao katika mazingira magumu
na hatarishi na kwamba, wanachangamotishwa kuwa makini katika matumizi ya rasilimali
iliyoko majini, ili iweze kuwa ni kwa mafao ya wengi.
Sekta ya uvuvi nchini
Ufilippini imeathirika kwa kiasi kikubwa baada ya kukumbwa na tufani iliyopelekea
maafa makubwa ya maisha na mali za watu. Hii ni Jamii inayohitaji kuonjeshwa mshikamano
wa upendo na ukarimu, ili iweze kuanza tena maisha kwa matumaini pasi na kukata tamaa!
Baraza
la Kipapa la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum katika ujumbe wake kwa Maadhimisho
ya Siku ya Wavuvi Kimataifa, linasema, nyakati hizi dunia inaendelea kushuhudia mashindano
ya kutafuta faida kubwa, hali ambayo imepelekea wavuvi wengi kufanya kazi katika mazingira
magumu na hatarishi, hali inayosababisha ajali za mara kwa mara na kwamba, wavuvi
ni Jamii ya watu ambao kwa sehemu kubwa haina hifadhi za kijamii.
Wavuvi wengi
wanafanya kazi bila ya kuwa na mikataba ya kazi; wanapewa misharaha "kiduchu" ambayo
haikidhi mahitaji msingi ya wavuvi pamoja na familia zao. Ni Jamii inayofanya kazi
kwa masaa mengi bila ya kukutana na kuonana na familia zao, hali ambayo inakwamisha
malezi, ustawi na maendeleo ya familia nyingi za wavuvi. Sekta ya uvuvi inatoa ajira
kwa wavuvi ambao hawana elimu kubwa na matokeo yake wanakosa sauti ya kudai haki zao
msingi na hivyo daima wanajikuta wakiwa pembezoni mwa Jamii nyingi.
Katika
ulimwengu wa utandawazi, Sekta ya Uvuvi imejikuta ikikabiliana na ukosefu wa wafanyakazi,
jambo ambalo limepelekea dhuluma, unyonyaji na unyanyasaji wa wavuvi, ambao wengi
wao ni wale wanaopatikana kutokana na biashara haramu ya binadamu, wakimbizi na wahamiaji
wanaotafuta nafuu na ubora wa maisha ughaibuni. Wavuvi wamekuwa pia wakishirikishwa
katika biashara haramu ya binadamu kwa kutumia vyombo vyao vya uvuvi.
Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alipokuwa anazungumza na washiriki wa
Kongamano la la XXIII la Wavui Kimataifa, lililofanyika mjini Vatican kunako mwaka
2012, aliwataka wavuvi kuhakikisha kwamba, wanalinda utu na heshima yao; wazingatie
usalama kazini; walinde na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia; sanjari na
kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, daima wakiwa mstari wa mbele kutetea
utu na heshima ya kila binadamu na kwamba, daima Kanisa liko pamoja nao!
Utume
wa bahari unapenda kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti kwa kufichua matatizo
na hali ngumu wanayokabiliana nayo wavuvi wanapokuwa kazini pamoja na changamoto zinazozikumba
familia zao wanapokuwa mbali na makazi yao. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha
kwamba, wavuvi wanakuwa na mazingira bora na salama ya kazi; wanapata tiba, matibabu
na muda wa kutosha kwa ajili ya mapumziko; mikataba ya kazi pamoja na hifadhi za kijamii
kama ilivyo kwa wafanyakazi kutoka katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii.